Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Bi. Seriel Mchembe
mara baada ya kuwasili wilayani humo (Juni 3, 2017) kwa ziara ya kikazi ya siku
moja. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Stephen Kebwe. (Picha na OWM).
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa Jimbo la Gairo, Bw. Ahmed
Shabiby mara baada ya kuwasili wilayani humo (Juni 3, 2017) kwa ziara ya kikazi
ya siku moja. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Stephen Kebwe
nawa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Bi. Seriel Mchembe (Picha na OWM).
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Bw.
Cliford Tandari mara baada ya kuwasili wilayani humo (Juni 3, 2017) kwa ziara
ya kikazi ya siku moja. Wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mvomero. (Picha na
OWM).
Viongozi
na watumishi wa Wilaya ya Gairo wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
(hayupo pichani) katika mkutano aliouitisha mjini Gairo Juni 3, 2017. (Picha na
OWM).
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi na watumishi wa Wilaya ya Gairo
(hawapo pichani) katika mkutano aliouitisha mjini Gairo Juni 3, 2017 (Picha na
OWM).
..........................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro,
Bw. Clifford Tandari aitishe kikao na uongozi wa Halmashauri ya Kilosa na
kupata kauli yao ni lini watalipa zaidi ya sh. milioni 210 wanazodaiwa na
Halmashauri ya Gairo.
“Katibu Tawala itisha kikao cha Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkuu wa Wilaya
na Mkurugenzi wa Halmashauri, waseme ni lini watazileta fedha hizo ambazo
zilitumwa kwao wakati Halmashauri ya Wilaya ya Gairo ikiwa haijafungua akaunti
zake,” alisema.
Ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Juni 3, 2017) wakati akizungumza na
viongozi wa mkoa wa Morogoro, wilaya ya Gairo na watumishi wa Halmashauri ya
Gairo mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa na wilaya katika kikao
kilichofanyika Gairo mjini
“Kilosa ni lazima wazilipe hizo fedha. Katibu Tawala simamia zoezi hilo
na kama watachelewa, uzikate moja kwa moja kwenye fedha yao wanayoletwa kutoka
Ofisi ya Rais (TAMISEMI). Nataka nipewe taarifa ya maamuzi hayo kabla Juni
haijaisha,” alisema.
Mapema akitoa taarifa ya wilaya hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Bi. Siriel
Mchembe alisema wanaidai Halmashauri ya Kilosa sh. 233,228,679 ambazo
ziliingizwa huko wakati wilaya hiyo inaanzishwa na hawakuwa wamefungua
akaunti ya wilaya.
“Fedha hizi zilikuwa zinapitia Kilosa wakati wilaya ya Gairo imeanzishwa
kwa kuwa kipindi hicho wilaya ya Gairo ilikuwa bado haijafungua akaunti. Fedha
hizi zinajumuisha ruzuku ya uendeshaji, mapato ya ndani na miradi ya
maendeleo,” alisema.
Alisema Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) iliagiza
wilaya ya Kilosa ilipe deni hilo kabla ya Juni 2016 lakini hadi sasa
wameshalipa sh. milioni 20 tu ambapo sh. milioni 10 zililipwa Desemba 2015 na
nyingine milioni 10 zililipwa Mei 2017.
Akisisitiza kuhusu makusanyo ya mapato, Waziri Mkuu amewakumbusha
watumishi hao kuwa Serikali imekwishatoa agizo la kutumia mashine za
kielektroniki kukusanya mapato ifikapo Julai mosi.
“Makusanyo ya mapato ya ndani ni eneo muhimu sana. Tumeshaagiza, mwisho
wa kutumia mifumo ya kawaida ni Juni 30. Kuanzia Julai mosi, kila eneo ni
lazima litumie mashine za kielektroniki,” alisema Waziri Mkuu.
Alihoji ni kwa nini Halmashauri ya Gairo ililenga kukusanya sh.milioni
889.5 lakini kufikia Aprili mwaka huu, makusanyo halisi yalikuwa ni sh. milioni
356.2 sawa na asilimia 40.
Alitumia fursa hiyo kuwapongeza Mamlaka ya Mapato (TRA) ya wilaya hiyo
ambao hadi kufikia Aprili, 2017 wameweza kukusanya sh. milioni 601.5 ikilinganishwa
na makadirio yao ya kukusanya sh. milioni 471 kwa mwaka.
Waziri Mkuu
aliwapongeza kwa sababu wamevuka lengo kwa asilimia 127.6.
Waziri Mkuu ambaye yuko kwenye ziara ya siku ya wilaya hiyo, asubuhi
alipanda mti kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ikiwa maadhimisho ya siku ya
upandaji miti hapa nchini.
Pia alikagua mradi wa maji wa kijiji cha Chakwale, na mradi wa visima 10
ambayo imekuwa na mgogoro kwa muda mrefu. Pia atazungumza na wananchi wa Gairo
mjini kwenye mkutano wa hadhara.
No comments:
Post a Comment