Waziri
Mkuu, Kasssim Majaliwa akizungumza katika kilele cha Mashindano ya 18 ya Afrika
ya Kuhifadhi Qur-an Tukufu yaliyofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es
salaam Juni 11, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika
kilele cha Mashindano ya 18 ya Afrika ya kuhifadhi Qur-ani Tukufu yaliyofanyika
kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juni 11, 2017, (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi , Mohammed Abdullah Aden (12) wa Somalia hundi
ya shilingi milioni 15, 750,000/= mshindi wa kwaza wa mashindano ya 18 ya
Afrika ya Kuhifadhi Qur-an Tukufu yaliyofanyika kwenye uwanja wa Taifa
jijini Dar es salaam Juni 11, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
.............................
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka waandaaji wa mashindano ya kuhifadhi
Qur ani ya Afrika ambao ni Taasisi ya Al-Hikma waangalie uwezekano wa
kuboresha zawadi kwa kutoa scholarships
(udhamini) kwa washindi au washiriki, hususan kwa washiriki wa Tanzania.
“Ongeeni na nchi marafiki kama
Saudi Arabia, waone uwezekano wa kutoa zawadi za ufadhili kwenye masomo ya
sekta za kimkakati kama vile mafuta na gesi, ili kuongeza hamasa na chachu ya
vijana walioko kwenye sekondari zetu nao waone fursa hii na kuichangamkia,
badala ya mashindano kujikita kwenye madrasa peke yake,” alisema.
Waziri Mkuu pia aliwataka wazazi wafuatilie nyendo za vijana wao ili
wasijiingize kwenye matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vingine viovu
vinavyoweza kuhatarisha maisha yao na ustawi wa nchi yetu kwa ujumla huku akisisitiza
pia waisaidie Serikali katika mapambano yake dhidi ya rushwa na ufisadi.
“Endeleeni kushirikiana na
Serikali katika mapambano yake dhidi ya rushwa na ufisadi na kuwafichua wakwepa
kodi. Kila mmoja wetu ahakikishe analipa kodi stahiki kwa mujibu wa sheria. Hii
itasaidia Serikali kuboresha huduma kwa wananchi ili waweze kufanya ibada zao
vizuri zaidi,” amesema.
Katika mashindano hayo mtoto wa miaka 12 kutoka Somalia, Mohammed
Abdullahi Aden ameibuka kidedea na kitita cha dola za Marekani 7,000 (sawa na
sh. milioni 15,750,000) katika mashindano ya 18 ya Afrika ya kuhifadhi Quran
kwenye kundi la washiriki wa juzuu 30.
Mohammed ambaye ni miongoni mwa washiriki wadogo zaidi wawili kuliko wote
(mwenzake anatoka Burundi), amejishindia pia IPAD, cheti, kompyuta iliyotolewa
na Balozi wa Kuwait, ahadi ya sh. milioni moja kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam na ahadi ya kwenda nchi yoyote aitakayo kutoka kwa kampuni ya Sky Bus
Travel Agency ya jijini Dar es Salaam.
Washindi wengine kwenye kundi hilo na umri wao kwenye mabano ni
Abdulkarim Ahmed Farhina (22) wa Sudan ambaye ameshinda dola za Marekani 5,000,
cheti, IPAD, kompyuta iliyotolewa na Balozi wa Kuwait, ahadi ya sh. milioni
moja kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Wa tatu ni Mahamoud Ali Chamfi wa Comoro (18) na Seif Ramadhani Zombe
(18) kutoka Taasisi za Tanzania ambao wote wamepata dola za marekani 3,000,
cheti, IPAD, kompyuta iliyotolewa na Balozi wa Kuwait, ahadi ya sh. milioni
moja kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Wa nne ni Khalil Mussa Hussein (17) kutoka Tanzania Bara ambaye amepata
dola za marekani 1,500, cheti, IPAD, na ahadi ya sh. milioni moja kutoka kwa
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Wa tano ni Ismail Issa Qasim (17) kutoka
Tanzania Visiwani ambaye dola za marekani 1,000, cheti, IPAD, na ahadi ya sh.
milioni moja kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Washiriki wengine kwenye kundi la juzuu 30 walitoka nchi za Nigeria,
Kenya, Uganda, Djibouti, Afrika Kusini, Rwanda, Ghana, Ethiopia, Congo DRC,
Burundi na Msumbiji. Umro wao ulikuwa ni kati ya miaka 12 na 26.
Washiriki wengine waliopewa zawadi ni wale walioweza kuhifadhi Juzuu tatu
(washindi watano), Juzuu tano (washindi watatu); Juzuu 10 (washindi watatu) na
Juzuu 20 (washindi watatu).
Viongozi wengine waliohudhuria kilele hicho ni Rais Mstaafu wa awamu ya
pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Makamu wa Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dk.
Mohammed Gharib Billal, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Balozi wa
Saudi Arabia nchini Tanzania, Mhe. Mohamed Bin Mansour Al Malek. Wengine ni
wawakilishi wanne wa Imam Mkuu wa Mskiti Mtakatifu wa Makkah, Sheikh Abdul
Rahman Ibn Abdul Aziz as-Sudais; Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh
Abubakar Zubeir bin Ally na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad
Mussa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Meya wa Temeke, Bw.
Abdallah Chaurembo kesho (Jumatatu, Juni 12, 2017) afuatane na Mkurugenzi wa
Manispaa hiyo, Bw. Nassib Mmbaga hadi kwenye kiwanja kilichopo eneo la Matumbi
na kukagua kama kuna uwezekano wa kuliongeza kwa taasisi ya Al-Hikma na wampe
majibu Jumanne kwani limekaa wazi kwa muda mrefu licha ya kuwa walishaliomba na
hawakupata majibu.
“Mstahiki Meya wa Temeke na Mkurugenzi wako, kesho Jumatatu nendeni
mkaangalie eneo husika kama linafaa kuongezwa na mfanye maamuzi. Eneo hilo
limekaa wazi kwa muda mrefu, na hawa wanataka wanataka kujenga zahanati.
Jumanne asubuhi nipate taarifa ya maamuzi yenu,” alisema Waziri Mkuu na
kushangiliwa na maelfu ya waumini waliokuwepo kwenye hafla hiyo.
No comments:
Post a Comment