Saturday, June 3, 2017

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE ASISITIZA AMANI KIBITI.

MWEN
Na Mwamvua Mwinyi,Kibiti

KIONGOZI wa mbio za mwenge kitaifa ,Amor Hamad ,amewaasa wananchi wa Kibiti -Pwani ,kupendana na kuachana na vitendo vinavyoondosha amani ili kuendelea kufanyakazi zao za kimaendeleo na kiuchumi .

Aidha aliwataka walimu katika shule mbalimbali wilayani hapo,kuhubiri amani na uzalendo kwa wanafunzi ili waweze kuwa mabalozi ndani ya jamii .

Alisema endapo wanafunzi wataweza kutambua umuhimu wa amani na utulivu wataifikisha majumbani na hatimae kurejesha utulivu .

Amor aliyasema hayo ,wakati akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Mjawa na baadhi ya wananchi mara baada ya kuzindua jengo la nyumba za walimu sita.

Alisema uchumi katika eneo lolote huinuka kama wananchi wake wanashirikiana kwa umoja.

“Amani ikidumishwa kila mwananchi atatekeleza majukumu yake kikamilifu ,bila hofu yoyote ” alieleza kiongozi huyo .

Amor alieleza kwamba,zipo baadhi ya nchi ikiwemo Syria ,Sudan ,Congo ambazo zilipitiwa na ukosefu wa amani suala lililosababisha kudidimia kwa maendeleo .

Alieleza, kutokana na hilo, haina budi kukemea vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani na utulivu kwenye maeneo yetu .

Pia alimuagiza mkuu wa wilaya ya Kibiti ,Gulam Kifu kusimamia changamoto za ukosefu wa maabara ,viti vya walimu na jengo la utawala katika shule ya sekondari Mjawa ,”kero ambazo ziliwasilishwa kupitia ujumbe wa mabango waliokuwa wamebeba wanafunzi”.

Amor alikemea suala la utoaji rushwa ,matumizi ya madawa ya kulevya na kudai madawa hayo yanapoteza nguvu kazi ya taifa.

Hakusita kuzungumzia mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria na ukimwi ,ili kulinda afya za watu .

Awali akipokea mwenge wa Uhuru kutoka Mafia , mkuu wa wilaya ya Kibiti ,Gulam Kifu ,alisema mwenge wa Uhuru ,ulitembelea miradi saba iliyogharimu bil 2.288.9.

Kifu ,alieleza kuwa ,kati ya fedha hizo ,nguvu za wananchi wamechangia bil.2.122 ,halmashauri sh .mil .3.5 na serikali kuu mil.37.4 .

Akizungumzia masuala ya kiusalama aliwatoa hofu wananchi na kuwaomba waendelee na shughuli zao kwani ulinzi upo wa kutosha wa askari Polisi na jeshi .
June mosi mwenge huo mwaka huu,ulianza mbio zake mkoani Pwani ,kwa kutembelea miradi saba wilaya ya Mafia ,iliyogharimu zaidi ya sh.bil 36.2,June 3 utakuwa Rufiji .

Jumla ya miradi 81 yenye thamani ya sh .bil 225.1 mkoani humo, itapitiwa na mbio za mwenge katika wilaya saba .

No comments:

Post a Comment