Tuesday, June 27, 2017

MADEREVA DAR-BAGAMOYO WALALAMIKIA KITUO CHA TEGETA NYUKI.

Wamiliki na madereva wa mabasi yanayofanya safari Dar-Bagamoyo wamelalamikia miundombinu ya kituo cha Tegeta Nyuki kuwa sio mizuri kwa kuingiza magari kituoni hapo.

Wakizungumza na wanaadishi wa Habari kituoni hapo, Madereva hao walisema kituo hicho hakijaandaliwa kwa matumizi ya mabasi mengi, na kwamba kuhamishia mabasi ya Bagamoyo kituoni hapo ni kuleta usumbufu.

Wakitaja baadhi ya mapungufu yaliyopo katika kituo hicho walisema ni pamoja na ubovu wa eneo lote la kituo kwakuwa limechimbika na kusababisha mashimo yanaopelekea kujaa maji wakati wa mvua na kusababisha usumbufu kwa abiria na magari yanayoingi humo.

Aidha, walisema Geti la kuingilia magari kuna shimo kubwa linalosababisha magari kukwama wakati wa kuingia, kukosekana kwa taa usiku uchache wa vyoo pamoja na udogo wa eneo leneyewe la kituo hicho.

Malalamiko ya madereva hao yamekuja kufuatia amri ya kuwataka kuondoka katika kituo cha makubusho na kuwataka kuishia kituo cha Tegeta nyuki.

Katika Barua iliyoandikwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi kavu na Majini (SUMATRA) iliyoandikwa Tarehe 19 Juni 2017 yenye Kumb: DA 218/280/02 iliwataka wamiliki wa mabasi ya Dar-Bagamoyo kuanza safari zake Tegeta Nyuki- Bagamoyo kama leseni zao zinavyoonyesha na sio kwenda Makumbusho, na  kwamba utaratibu huo umetakiwa kuanza rasmi kuanzia Tarehe 26 Juni 2017.
 
Awali mwaka 2012 Umoja wa Maendeleo ya Madereva Dar es Salaam-Bagamoyo(UMAMADARBA) waliindikia Wizara ya Uchukuzi (wakati huo) na kulalamikia lesena zilizotolewa na SUMATRA za kuwataka kushia Tegeta Nyuki badala ya Mwenge.

Katika Barua yao hiyo yenye Kumbukumbu Namba UM/D/B/008/2012 YA Tarehe 14 Novemba 2012, Umoja wa Maendeleo ya Madereva walilalamikia pamoja na mambo mengine ubovu wa kituo cha Tegeta Nyuki na kuiomba Wizara ya uchukuzi iingilie kati kutatua mgogoro huo ikiwa ni pamoja na kutengeneza kituo cha Tegeta Nyuki au kuwaruhusu waendelee kituo cha Mwenge (kwa wakati huo)

Kufuatia Barua hiyo ya Umoja wa Maendeleo ya Madereva, Wizara ya uchukuzi iliwajibu katika Barua iliyoandikwa Tarehe 04 Disemba 2012 yenye Kumbukumbu Namba CA 414/505/01/55, kwamba madereva wanapaswa kukubali leseni za Tegeta nyuki kutokana na uwezo mdogo wa kituo cha Mwenge, pamoja na kupisha mradi wa mabasi yaendayo haraka DART ambayo yalitarajiwa mpaka kufikia mwaka 2014 kukamilika hadi Tegeta.

Katika Barua hiyo ya Wizara iliwataka iliwataka Madereva wa Dar- Bagamoyo kutumia vibali maalum vitakavyowafikisha Mwenge na Makumbusho kwa sasa mpaka kituo cha Tegeta Nyuki kitakapokamilika kutengenezwa.

Kwa upande wao umoja wa Maendeleo ya Madereva Dar es Salaam-Bagamoyo walisema kwa mujibu wa Barua ya Wizara ya uchukuzi ambayo iliwataka wasubiri kituo cha Tegeta Nyuki kitengezwe na kwamba hoja ya kuwahamishia tegeta Nyuki ni kupisha Mradi wa mabasi ya haraka DART ifikapo mwaka 2014, bado vyote hivyo havijakamilika na kwamba bado wanaiomba SUMATRA kurejea barua ya Wizara ya Uchukuzi  ili waweze kuwaruhusu kurejea makubusho au vinginevyo.
 
Akizungumza na Madereva, Wamiliki wa Mabasi ya Dar- Bagamoyo pamoja na Waandishi wa Habari, katika kituo cha Tegeta Nyuki, Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani, mkoa wa kipolisi Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP-Theopista Malya alisema, Madereva wanapaswa kuzingatia leseni zao na kwamba hawapaswi kuto huduma ya usafiri kinyume leseni zao.

Aliongeza kuwa, Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama Barabarani kazi yake ni kuhakikisha Madereva wanatii sheria za usalama Barabarani ikiwa ni pamoja na kufanya safari kwa mujibu wa leseni ya gari husika au kibali maalum cha SUMATRA na si vinginevyo.

Nae Diwani wa kata ya Kunduchi Mh. Michael Urio akizungumza na mwandishi wa Habari hizi kuhusiana na kadhia hiyo alisema anafahamu changamoto zilizopo katika kituo hicho na kwamba tayari zimeanza kufanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na kurekebisha mashimo yaliyomo ndani ya kituo hicho.
 

No comments:

Post a Comment