Serikali imesema inaendelea kupitia sheria, kanuni na taratibu za
misamaha ya kodi mwaka hadi mwaka ili kuhakikisha kuwa misamaha yote isiyokuwa
na tija inafutwa na hivyo kuiwezesha Serikali kuongeza mapato kwa ajili ya
kupeleka huduma za maendeleo kwa wananchi wake.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali la Msingi la
Mbunge wa Masasi, Mhe. Rashid Mohamed Chuachua (CCM), aliyetaka kujua namna
Serikali inavyodhibiti misamaha ya kodi tangu irekodiwe kwa viwango vya juu
Mwaka wa Fedha 2011/2012.
Mhe. Chuwachuwa alihoji mwenendo wa utoaji wa misamaha ya kodi kwa
wawekezaji kwa maelezo kuwa Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi zilizopoteza
fedha nyingi kwa ajili ya misamaha ya kodi ikilinganishwa na nchi
nyingine za Afrika Mashariki kwa kigezo cha kuvutia Wawekezaji.
Alisema kuwa kwa mujibu taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali ya mwaka 2009-2010, Tanzania ilipoteza asilimia 15 ya Pato la Taifa
lililotarajiwa kukusanywa kutokana na misamaha ya kodi, mwaka 2010-2011
asilimia 8, kwa mwaka 2011-2012 asilimia 27 ya mapato ya Serikali
yalipotea.
“Je hali ya misamaha ya kodi kuanzia 2013-2014 hadi sasa ikoje’’. Alihoji
Mhe. Chuachua.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu
Kijaji (Mb), alisema misamaha ya kodi kama sehemu ya asilimia ya Pato la Taifa
katika kipindi cha kuanzia mwaka 2013/14 hadi sasa imekuwa ikipungua mwaka hadi
mwaka.
“Misamaha hiyo ilikuwa asilimia
2.2 ya Pato la Taifa mwaka 2013/14, asilimia 1.9 ya Pato la Taifa katika mwaka
2014/15 na asilimia 1.1 ya Pato la Taifa katika mwaka 2015/16” Alifafanua Dkt. Kijaji.
Aidha aliongeza kuwa misamaha ya kodi ikilinganishwa na mapato ya kodi
imekuwa ikipungua kutoka asilimia 18 ya mwaka 2013-2014 hadi kufikia asilimia
8.6 ya mapato yote ya kodi katika mwaka 2015-2016.
Dkt. Kijaji alifafanua kuwa misamaha ya kodi inatolewa na Serikali kwa
mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za kodi zilizopo, huku kukiwa na baadhi ya
huduma zinazotolewa katika jamii ambazo hazistahili kulipiwa kodi kwa sababu
hazina manufaa ya kibiashara.
‘’Pamoja na hatua nzuri zinazochukuliwa na Serikali za kupunguza misamaha
ya kodi ni vema ikafahamika kwamba si kila msamaha wa kodi una madhara hasi
katika jamii na uchumi kwa ujumla’’. Alisema Dkt. Kijaji.
Alitolea mfano wa mashirika ya dini yanayopata misamaha ya kodi kwa
mujibu wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) (2014), kwa sababu huduma
zinazotolewa na taasisi hizo hazina faida ya kibiashara kama ilivyo kwa kampuni
za kibiashara.
Katika swali la nyongeza Mbunge huyo, alitaka kujua mpango wa Serikali
kuhusu misamaha ya kodi kwa mwaka wa fedha 2017-2018.
Akijibu swali hilo la nyongeza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Kijaji, alimuomba Mhe. Chuachua awe na subira hadi tarehe 8 mwezi huu
ambapo Serikali itapeleka mapendekezo yote katika Bunge, ili mapendekezo
hayo yaweze kujadiliwa na kupitishwa na Bunge.
No comments:
Post a Comment