Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Sheikh Nurdin Kishik ambaye ni Mhadhiri wa
Kimataifa wa Dini ya Kiislaam, (kulia) na ujumbe wake, ofisini kwake bungeni
mjini Dodoma Juni 2, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kushiriki katika sala ya Ijumaa
kwenye Msikiti wa Al- Gadaf mjini Dodoma Juni 2, 2017. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
..........................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kuliombea
Taifa ili liendelee kudumu katika hali ya amani na utulivu.
Alisema suala la kudumisha amani na utulivu ni jukumu la kila mmoja,
hivyo kila mwananchi kwa imani yake ahakikishe anashiriki kutunza hali hiyo.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Juni 2, 2017) baada ya kumaliza
kuswali sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Al-Gadaf, mjini Dodoma.
Alisema ni vema kila mwananchi akajivunia hali ya amani na utulivu
iliyoko nchini kwa kuwa ndiyo inayowezesha kufanyika kwa shughuli mbalimbali za
kimaendeleo. “Tuendelee kudumisha amani, tufanye ibada kila mtu kwa imani yake.
Serikali inaheshimu dini zote kwa sababu ndizo zinazojenga amani na
mshikamano,” alisema.
Pia amewataka wazazi wahakikishe wanawalea watoto wao katika mazingira ya
kidini ili wanapokuwa watu wazima waje kuwa raia wema. “Tuendelee
kuhamasisha watoto wetu wasikilize mahubiri ya dini; ni jukumu letu sisi kama
wazazi kuwahimiza wahudhurie mahubiri ya viongozi wa dini ili waweze kujijenga
vyema kimaadili na kiimani pia.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewakumbusha Waislamu
wahakikishe wanautumia vizuri mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa kuzidisha ibada na
kusaidia watu wenye mahitaji. “Leo ni Ijumaa ya kwanza katika mfungo wa mwezi
mtukufu wa Ramadhani, nawaomba tutumie vizuri mwezi huu ili tupate baraka,”
alisema.
Ibada hiyo ya sala ya Ijumaa iliongozwa na Sheikh Nurdin Kishki ambaye ni
Imamu wa Msikiti wa Vetenari, wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam.
Sheikh Kishki katika hotuba yake, aliwasisitiza Waislamu waendelee
kufanya mambo mema yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu ikiwemo kuwatunza wazazi
wao, kumswalia Mtume Mohammed (S.A.W) na kufunga katika mwezi mtukufu wa
Ramadhan.
No comments:
Post a Comment