Na Jumia
Travel Tanzania
Siku ya
Jumatatu ya Juni 5 itakuwa ni maadhimisho ya ‘Siku ya Mazingira Duniani’ ambayo
huadhimishwa na mataifa tofauti duniani ikiwa imebeba kauli mbiu ya
‘Kuwaunganisha Watu na Mazingira Asilia.’
Mapema wiki hii Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu
wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Mh. January Makamba
alitoa taarifa kwa umma kuwa kwa hapa nchini maadhimisho ya siku hiyo
kitaifa yatafanyika kijijini Butiama mkoani Mara, mahali alipozaliwa mwasisi wa
taifa la Tanzania, Hayati Mwl. Julius Nyerere, ikiwa ni kuenzi jitihada zake za
kulinda na kuhifadhi mazingira.
Katika kunogesha sherehe hizo Waziri huyo amesema
kuwa serikali imetoa ofa kwa wananchi kutembelea hifadhi yoyote ya mbuga ya
wanyama bila ya kiingilio chochote kwa siku tatu, kuanzia Ijumaa ya Juni 2
mpaka Jumapili ya Juni 4.
Alisema kuwa lengo kubwa ni kuona uwepo wa wanyama na
kujifunza kuwa mazingira yanahitaji kulindwa zaidi na zaidi.
Kauli hiyo
ya Waziri imekuja siku chache baada ya kampuni inayojihusisha na masuala ya
huduma za hoteli mtandaoni barani Afrika, Jumia Travel kuzindua kampeni ya
‘DemocratizeTravel’ inayolenga kuwakomboa waafrika na watanzania kiujumla
katika kusafiri na kutalii vivutio mbalimbali nchini huku wao wakirahisisha
huduma za malazi na hoteli.
Kampuni
hiyo inalenga kuhamasisha na kutoa elimu juu ya dhana potofu iliyojengeka
miongoni mwa wananchi ya kwamba mchakato mzima unaohusisha utalii ni gharama.
Katika kulifanikisha hilo kampuni hiyo imedhamiria kuelimisha juu ya vivutio
vilivyopo nchini, masuala ya msingi ya kuzingatia wakati wa kusafiri pamoja na
kurahisisha gharama za malazi kupitia hoteli za kila hadhi zilizopo kwenye
mtandao wao wa travel.jumia.com.
Baadhi ya
changamoto zilizopo ni pamoja na mwamko mdogo wa watanzania kutembelea vivutio
vya kitalii vilivyopo karibu na wanayoishi. Wapo baadhi yao hawafahamu kuwa
wanaishi na vivutio hivyo na wengine huchukulia mchakato mzima unahusisha
gharama kubwa.
Vifuatavyo
ni baadhi ya vivutio vya kitalii ambavyo watanzania mahali popote walipo
wanaweza kwenda kuvitembelea wikendi hii bure kabisa kwa mujibu wa kauli ya
serikali katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani.
Kanda ya
Kaskazini. Mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Mara kwa kiasi kikubwa imebarikiwa
kuwa na hali ya hewa nzuri inayowavutia watalii, hifadhi za mbuga za wanyama,
maeneo yenye masalia ya kale pamoja na milima ya kuvutia. Vivutio
vinavyopatikana huko ni kama vile; Hifadhi za Taifa za Arusha, Mkomazi, Ziwa
Manyara, Mlima Kilimanjaro, Serengeti na Ngorongoro.
Kanda ya
Magharibi. Eneo hili inapatikana mikoa kama vile ya Kigoma na Rukwa ambayo nayo
haijaachwa nyuma kwa upande wa vivutio vya kitalii.
Wananchi wanaoishi katika
au karibu na mikoa hii wanaweza kutembelea Hifadhi za Mbuga za Wanyama kama
vile; Gombe, Katavi, Mahale, Rubondo na Saanane na kujionea wanyama wengi
hususani sokwe wa kipekee.
Kanda ya
Kusini. Morogoro, Iringa, Mbeya na Ruvuma ni baadhi ya mikoa inayoweza
kupatikana katika ukanda huu ambapo kuna hifadhi za kitaifa kama vile; Kitulo,
Mikumi, Ruaha na Udzungwa. Mbuga kama vile Mikumi inajulikana kuwa na idadi
kubwa ya wanyama kama vile pundamilia, nyati na tembo.
Kanda ya
Mashariki. Ukanda huu kwa kiasi kikubwa umepakana na fukwe ya bahari ya Hindi
ambayo inapatikana kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Lindi na
Mtwara. Mbali na kuwa na hoteli nyingi zilizojengwa pembezoni mwa fukwe ya
bahari hiyo lakini pia mikoa hiyo inavyovivutio vingine lukuki kama vile;
Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Mji wa Bagamoyo, Kisiwa cha Kilwa, Mapango ya
Amboni na Mikindani.
Visiwa vya
Zanzibar. Hakuna anayeweza kubisha kuwa vivutio mbalimbali vilivyomo visiwani
humo hususani fukwe nyingi safi na za kuvutia pamoja na hoteli za kifahari
ndivyo huwatoa watu kutoka mataifa mbalimbali duniani kwenda kuzuru.
Mbali na
visiwa hivi kusifika kuwa na sehemu nzuri za kupumzika bali pia vina utajiri
mkubwa wa tamaduni za watu wa mataifa mbalimbali waliopata kuishi humo kama
vile Waarabu, Waingereza pamoja na waafrika kwa ujumla. Lakini pia kuna majengo
ya kale yaliyojengwa karne nyingi zilizopita ambayo mpaka leo hii bado yapo na
vinginevyo vingi.
Uzuri wa nchi ya Tanzania umebarikiwa kuwa na
vivutio vya kila namna karibuni kila mkoa. Hivyo kisingizio cha kutotembelea
sehemu fulani kwa sababu ipo mbali kinakuwa hakina mantiki, Jumia Travel
inakushauri anza kwanza na vilivyo karibu nawe na fursa hii iliyotolewa na
serikali inaweza kuwa ni mwanzo mzuri kwako.
No comments:
Post a Comment