KILOSA YAANZA MAANDALIZI YA KUKABILIANA NA EL NINO - DC SHAKA APIGA MARUFUKU MAFUNZO, AAGIZA FEDHA ZINUNUE VIFAA VYA DHARULA





Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Mhe. Shaka Hamdu Shaka ameongoza Kikao Maalum cha Kamati ya Maafa ya Wilaya kilichojumuisha Kamati ya Ulinzi na Usalama na wadau mbalimbali kujadili maandalizi ya kukabiliana na mvua kubwa za El Nino zinazotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).


Akifungua kikao hicho, Mhe. Shaka amesema Wilaya ya Kilosa imejifunza kutokana na athari za mafuriko ya miaka ya nyuma na safari hii maandalizi yote yatajikita kwenye vitendo, sio kwenye makaratasi.


Amefafanua kuwa uamuzi huo ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyeagiza mikoa na wilaya zote kuchukua tahadhari mapema na kuhakikisha taarifa za TMA hazibaki kwenye makaratasi bali zinafuatwa na hatua za vitendo.


Akizungumza kwa msisitizo, DC Shaka alisema:


_"Wilaya ya Kilosa tumeamua fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya maafa zitanunua vifaa vya dharura vinavyoonekana. Sitaki kusikia mafunzo, semina na warsha. Wananchi wa Kilosa wanajua mafuriko ni nini. Wanachohitaji ni boti la kuwaokoa, blanketi la kujifunika na dawa wakiumwa."_


_"Nimesikia kuna fedha zimetengwa kwa ajili ya mafunzo ya maafa. Sitaki kusikia mafunzo. Sitaki kabisa. Nani hapa Kilosa hajui mafuriko? Mtoto wa miaka 10 wa Kimamba anajua mafuriko kuliko mtaalamu. Fedha zozote za maafa zisiguse mafunzo."_


_"Mafuriko yakija kesho, hutamwambia mama aliyekwama na watoto wawili juu ya paa - 'Mama subiri nikupe brochure ya mafunzo'. Hapana. Utamwambia - 'Mama panda boti, hili hapa blanketi, huu hapa mchele'."_


Kwa upande wao, wadau mbalimbali walioshiriki kikao hicho wamepongeza utaratibu wa Wilaya ya Kilosa wa kushirikisha makundi yote na kueleza kuwa mipango iliyopangwa itatekelezeka na kuhakikisha usalama wa wananchi katika kipindi hiki cha tahadhari.


Kikao kimeazimia kuanzishwa kwa Stoo ya Dharura ya Wilaya na kuhamishwa kwa wananchi wanaoishi maeneo hatarishi.



Comments

Popular posts from this blog

DC SHAKA AONGOZA KIKAO CHA KAMATI YA USHAURI YA KODI KILOSA

SILAHA 17 ZA MOTO ZASALIMISHWA TABORA

NDEJEMBI AAGIZA DAMPO LA PUGU LIBORESHWE.

GURUMO AMSHUKURU RAIS DKT. SAMIA NA WAZIRI KIKWETE

TAKUKURU KAGERA YAOKOA ZAIDI YA BILIONI 2.

RAIS WA ZANZIBAR ATOA POLE KUFUATIA KIFO CHA MAMA FATMA KARUME.

GREEN ACRES YAANZA KUFUNDISHA AKILI MNEMBA