DC WELLA APONGEZA USIMAMIZI MZURI MIRADI YA AFYA
DC WELLA APONGEZA USIMAMIZI MZURI MIRADI YA AFYA
Na Allan Kitwe, Tabora
MKUU wa Wilaya ya Tabora Upendo Wella ameeleza kufurahishwa na usimamizi mzuri wa miradi ya afya iliyotekelezwa katika Kata za Ipuli na Itonjanda katika halmashauri ya manispaa ya Tabora yenye thamani ya zaidi ya shilingi mil 700.
Akiongea na Wataalamu na Watendaji wa manispaa hiyo juzi DC ameeleza kuwa miradi ya afya iliyopelekwa katika Kata hizo imesimamiwa kwa weledi mkubwa na kukamilika kwa wakati na sasa wananchi wameanza kunufaika.
Amebainisha kuwa serikali inaleta fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji miradi ya maendeleo ambayo hugharimu mabilioni ya fedha, lakini utekelezaji umekuwa ukisuasua kwa baadhi ya miradi kwa sababu ya usimamizi mbovu.
‘Nawapongeza sana Wataalamu wetu akiwemo Mhandisi kwa kusimamia ipasavyo miradi hii iliyotekelezwa katika Zahanati ya Manoleo (Kata ya Itonjanda) na Kituo cha Afya Maili tano katika Kata ya Ipuli, mmefanya kazi nzuri sana’, ameongeza.
DC ametoa zawadi ya shilingi laki mbili kama motisha kwa Mhandisi wa manispaa hiyo kwa kuratibu na kusimamia vizuri miradi hiyo hali iliyopelekea thamani ya fedha kwenda sambamba na kazi iliyofanyika.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa manispaa hiyo Dkt John Pima ametaja miradi iliyotekelezwa kuwa ni jengo la kufulia nguo katika Zahanati ya Manoleo (Itonjanda) na upanuzi wa miundombinu katika Kituo cha Afya Maili 5.
Amefafanua kuwa mradi wa Manoleo ulitengewa shilingi mil 50 lakini kutokana na uratibu na usimamizi mzuri wa Mganga Mfawidhi na Kamati ya Ujenzi zitakatumika sh mil 43 tu na kubakia kiasi cha sh milioni 7.
Na mradi wa upanuzi wa Kituo cha Afya Maili 5 ulitengewa shilingi mil 675 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya akinamama, jengo la mionzi (x-ray), kichomea taka, mfumo wa maji taka na kuweka umeme, kazi hii imekamilika kwa asilimia 100.
‘Kwenye mradi huu zimetumika shilingi mil 550 na kubakia sh mil 125, kutokana na uratibu na usimamizi mzuri, hili ni jambo la kujivunia sana, hawa wote tunawapatia cheti cha pongezi kwa kazi nzuri waliyofanya’, alisema.
Diwani wa Kata ya Ipuli Molo Juma Molo amemshukuru DC, Mkurugenzi na Mstahiki Meya kwa zawadi walizotoa kwa Watumishi wa Kituo cha Afya Maili 5 na Zahanati ya Manoleo, hii itawaongezea molari na kufanya kazi kwa kujituma vizuri zaidi.

Comments
Post a Comment