MRADI WA BOMBA LA MAFUTA KUANZA JANUARI 2027
Na Alodia Dominick,
Bukoba,
Mradi wa bomba la mafuta ambao utekelezaji wake wa jumla umefikia asilimia 87.7 unatarajia kukamilika na kuanza rasmi Januari 15,2027.
Mradi huo ambao mkataba wake ulisainiwa mwaka 2021 unatarajiwa kuanza rasmi ifikapo Januari 15, 2027 na kutokana na mkataba mradi utadumu takribani miaka 25.
Mratibu wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kusafirisha mafuta ghafi Afrika Mashariki (EACOP) Jumanne Saidi akitoa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari mkoani Kagera juu ya mradi wa bomba la mafuta na maendeleo yake ameeleza kuwa, mradi huo utaanza rasmi Januari 15,2027.
Amesema sh.bilioni 35.6 zimetumika kulipa fidia kwa wananchi wapatao 10,144 maeneo yote yanayopitiwa na bomba la mafuta na nyumba zilizoguswa ni 340, kwa Kagera ni nyumba 119 ambapo waguswa kwa Kagera wako 118.
"Mikoa inayopitiwa na bomba la mafuta ni nane ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Manyara, Dodoma na Tanga na katika mkoa wa Kagera unapita katika wilaya nne za Misenyi, Bukoba vijijini, Muleba na Biharamlo" amesema Saidi
Saidi amesema kuwa, mradi utakapoanza Tanzania itanufaika kwa kulipwa dola 12.77 kila pipa na yatakuwa yanavumwa mapipa 216,000 kwa siku moja
Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha uhusiano na mawasiliano Shirika la maendeleo ya petroli Tanzania (TPDC) Marie Nsellemu ameeleza kuwa, mkoa wa Kagera ni wa kwanza kwa kupitiwa na bomba la mafuta katika wilaya nne.
Nsellemu amesema, kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga mradi unakatiza kilomita 1,480 hivyo amewataka wananchi kulinda miradi inayofanywa na serikali kupitia TPDC.
Akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari Katibu Tawala msaidizi Isaya Tendega ameeleza kuwa, tangu mchakato mzima wa utafiti wa kimazingira ulipoanza kufanyika mpaka sasa mradi unaelekea mwisho mkoa wa Kagera umenufaika kwa sehemu kubwa kiuchumi.
"Kwanza kibisa ni ajira za moja kwa moja kwenye maeneo linapopita bomba la mafuta vijana, mama ntilie na wafanyabiashara, kumekuwa na hatua mbalimbali mfano hatua za utoaji wa ardhi ambapo sheria za kimataifa zimezingatiwa ili kuhakikisha kwamba mwananchi anapoondolewa kwenye eneo lake kupisha mradi basi anajengewa mazingira mazuri zaidi ya yale aliyokuwa nayo" amesema Tendega
Ameeleza kuwa, hilo limedhibitika kwani wapo waliokubali kujengewa nyumba bora zaidi na wapo waliopewa fedha taslimu kwenda kujenga wanapotaka wao.




Comments
Post a Comment