SHULE YA MSINGI IPULI YAPEWA TUZO YA UFANISI

 

SHULE YA MSINGI IPULI YAPEWA TUZO YA UFANISI


Na Allan Kitwe, Tabora


HALMASHAURI ya Manispaa Tabora imetoa tuzo maalumu ya pongezi kwa Uongozi wa Shule ya Msingi Ipuli iliyopo katika Kata ya Ipuli Mjini Tabora kwa usimamizi mzuri wa fedha za maendeleo zilizopelekwa shuleni hapo.


Akikabidhi tuzo hiyo (Cheti cha Pongezi) leo, Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Ghullam-Hussein Dewj amempongeza Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Chiku Mwaka na Kamati yake kwa kusimamia vizuri maboresho ya miundombinu.


Amesema kuwa Uongozi wa shule hiyo umeonesha weledi mkubwa kwa kusimamia kwa dhati mradi wa uboresha elimu (GPE) uliotekelezwa na serikali shuleni hapo kwa mwaka wa fedha uliopita kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 60.


‘Chini ya usimamizi wa Mwalimu Mkuu na Kamati ya Shule, Mradi umetekelezwa kwa ufanisi wa hali ya juu hali iliyopelekea mazingira ya shule hiyo kubadilika kwa kiasi kikubwa na kufanya watoto na wazazi kupenda shule yao’, ameeleza.    


‘Tunakupongeza sana Mwalimu Mkuu na Wasaidizi wako kwa kusimamia vizuri mradi huu, hakika mmeonesha weledi mkubwa, Kamati ilipita ili kukagua na kujionea maendeleo yake na kupendekeza mpewe tuzo hii’, amedokeza.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Dkt John Pima amepongeza shule hiyo kwa kutumia vizuri fedha za serikali na kuwataka wakuu wa shule zingine kuiga mfano huo huku akitoa onyo kwa watakaotumia vibaya fedha.


Amesisitiza kuwa fedha zote zinazotolewa na serikali kupitia halmashauri hiyo ni lazima zifanye kazi iliyokusudiwa kinyume na hapo hawatasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayebainika kuzitumia kinyume.


Akifafanua mradi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata hiyo ambaye ni Diwani wa Kata hiyo Molo Juma Molo amesema kuwa manispaa iliipatia shule hiyo takribani shilingi milioni 60 kwa ajili ya kuboresha miundombinu yake.


Fedha hizo zimejenga madarasa 2, ofisi ya walimu, matundu 3 ya vyoo, kichomea taka cha wasichana, kibuyu chirizi cha kunawia mikono na tenki la maji la lita 3000, fedha imetosheleza na chenji imebaki, ameongeza.





Comments

Popular posts from this blog

MWENGE WA UHURU, WAZINDUA NA KUTEMBELEA MIRADI YA MILIONI 900. BUKOBA

MAKAMU WA RAIS, ATEMBELEA OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA

TARURA YATENGA BIL. 1 KUKABILIANA NA EL NINO TABORA

MRADI WA BOMBA LA MAFUTA KUANZA JANUARI 2027

MANISPAA TABORA KULIPA MIL 27 ZA BODI YA MIKOPO