MBUNGE WA BAGAMOYO AKABIDHI TIKETI YA NDEGE KWA KIJANA MALICK SABABU
Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Mhe. CPA Subira Khamis Mgalu, amemkabidhi tiketi ya ndege kijana wa Bagamoyo, Ndg. Malick Sababu, kwa ajili ya safari yake ya kwenda nchini Urusi, ambako amepewa fursa ya kuendelea na masomo ya Shahada ya Uzamili (Master’s) katika fani ya Geolojia (Geology).
Malick Sababu ni kijana mwenyeji mkazi wa Bagamoyo kata ya Kiromo, ambaye amepata elimu yake katika Shule ya Msingi Kiromo, Ramiya Islamic Education Center kwa elimu ya Sekondari, na Bagamoyo Secondary School kwa elimu ya Kidato cha Tano na Sita.
Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), ambako alifanikiwa kupata Shahada yake ya kwanza.
Kwa juhudi na mafanikio yake katika masomo, Malick amepata nafasi ya kwenda nchini Urusi kwa udhamini wa Serikali ya Urusi kwa kipindi cha miaka minne, kwa ajili ya kuendelea na masomo ya Geolojia.
Hata hivyo, pamoja na kupata udhamini huo, safari ya kwenda Urusi ilihitaji baadhi ya gharama ambazo alipaswa kujigharamia, jambo lililomfanya akabiliwe na changamoto ya kupata tiketi ya ndege.
Kutokana na hali hiyo, Mhe. Subira Khamis Mgalu, kwa kutambua umuhimu wa kuwawezesha vijana kupata fursa za elimu na kwa kuzingatia kuwa Malick ni kijana wa Bagamoyo kutoka familia yenye kipato cha kawaida, ameamua kumsaidia kwa kumpatia tiketi ya ndege hadi nchini Urusi ili aweze kuanza safari yake ya masomo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, katika ofisi ya Mbunge Bagamoyo, Mhe. Mgalu amemtakia Malick safari njema na mafanikio katika masomo yake, huku akimtaka kutumia fursa hiyo kwa bidii, nidhamu na kujiamini, ili baada ya masomo aweze kurejea nchini na kutumia taaluma yake katika kuchangia maendeleo ya Bagamoyo na Tanzania kwa ujumla.
“Bagamoyo tunakutegemea. Nenda ukasome kwa bidii, ukaitangaze Bagamoyo na Tanzania kwa kufanya vizuri. Tunatarajia utakapomaliza masomo yako utarejea na kuitumia elimu yako kulijenga Taifa letu,” amesema Mhe. Mgalu.
Msaada huo unaendelea kuonesha dhamira ya Mhe. Subira Mgalu ya kuwawezesha vijana wa Bagamoyo kutumia fursa za elimu, kukuza vipaji na kujenga uwezo utakaowasaidia wao binafsi pamoja na jamii na Taifa kwa ujumla.
Tunamtakia Malick Sababu safari njema na kila la kheri katika masomo yake nchini Urusi. Bagamoyo inajivunia vijana wake.



Comments
Post a Comment