MANISPAA TABORA YAASWA KUONGEZA MAPATO

 

MANISPAA TABORA YAASWA KUONGEZA MAPATO


Na Allan Kitwe, Tabora


HALMASHAURI ya Manispaa Tabora imetakiwa kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato katika vyanzo vyake ili kufanikisha utekelezaji miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata zake zote.


Wito huo umetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Tabora Upendo Wella alipokuwa akizungumza na watalaamu, watendaji, madiwani, viongozi wa chama, wawakilishi wa taasisi na vyombo vya ulinzi na usalama.


Wella ameeleza kuwa licha ya kwamba serikali inapeleka fedha nyingi katika halmashauri zote kwa ajili ya utekelezaji miradi ya maendeleo, halmashauri hazipaswi kubweteka, zinatakiwa kujiongeza kwa kukusanya mapato zaidi.


‘Mapato ya halmashauri ni muhimu sana kwa kuwa yanasaidia kuharakisha utekelezaji miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ikiwemo kukamilisha miradi yote inayoanzishwa katika kila kata’, amedokeza.


Amesisitiza kuwa kusuasua kwa baadhi ya miradi katika vijiji, mitaa na kata kunachagiwa na ufinyu wa bajeti lakini kama halmashauri itakuwa na mapato ya kutosha hakuna mradi hata mmoja utakaolala.


‘Naomba tuongeze kasi ya ukusanyaji mapato katika halmashauri yetu ili kuharakisha maendeleo ya wananchi, nataka kila mtumishi asimame kwenye zamu yake na kutekeleza wajibu wake ipasavyo’, ameasa.


Aidha DC Wella ameagiza wataalamu, watendaji na waheshimiwa madiwani kuhakikisha suala la usafi linapewa kipaumbele katika maeneo yao, huku akibainisha kuwa atapita katika maeneo yote ili kujionea hali ya usafi.


‘Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameonesha kukerwa na mazingira ya uchafu katika Miji mbalimbali hapa nchini na kuagiza Wakuu wa Mikoa kusimamia ipasavyo suala hilo, Tabora Mjini nataka tuwe mfano’, amesema.


Aidha ametoa wito kwa halmashauri na wananchi wote kuchukua tahadhari ya mvua za el nino kama ilivyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa kuwa mwezi Oktoba, Novemba na Desemba kutakuwa na mvua nyingi ili kuepuka madhara yatokanayo na mvua hizo.





Comments

Popular posts from this blog

MWENGE WA UHURU, WAZINDUA NA KUTEMBELEA MIRADI YA MILIONI 900. BUKOBA

MAKAMU WA RAIS, ATEMBELEA OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA

TARURA YATENGA BIL. 1 KUKABILIANA NA EL NINO TABORA

SHULE YA MSINGI IPULI YAPEWA TUZO YA UFANISI

MRADI WA BOMBA LA MAFUTA KUANZA JANUARI 2027

WMA: KILO NA LITA YA TANZANIA NI KILO NA LITA YA DUNIA

BAKWATA YATANGAZA SIKUKUU YA MAULIDI NI TAREHE 25 AGOSTI 2026