THE ISLAMIC FOUNDATION YAMKABIDHI CHEREHANI ALIYEMALIZA KIFUNGO GEREZANI.

 

Taasisi ya The Islamic Foundation yenye Makao yake Makuu Mkoa wa Morogoro imetoa msaada wa cherehani kwa Issa Mohamed Kitambi, aliyemaliza kifungo cha miaka minane katika Gereza la Mahabusu Morogoro, ikiwa ni sehemu ya kumuunga mkono katika kuanza maisha mapya baada ya kutoka gerezani.


Issa ambaye alipata mafunzo ya ushonaji akiwa gerezani, sasa anatarajiwa kutumia cherehani hiyo kuendeleza ujuzi alioupata na kujiajiri kupitia kazi ya ushonaji wa nguo.


Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa The Islamic Foundation, Arafat Badru, amesema wameguswa na jitihada zinazofanywa na Jeshi la Magereza za kuwapatia wafungwa mafunzo ya ujuzi, ili wanapomaliza vifungo vyao wawe na uwezo wa kujitegemea.


Amesema cherehani hiyo imelenga kumpa Issa nyenzo ya kuanzia katika kazi yake na kumsaidia kuendesha maisha yake baada ya kumaliza kifungo.


Akizungumza katika zoezi hilo, Mkuu wa Gereza la Mahabusu Morogoro, Mrakibu wa Jeshi la Magereza (SP) SabaSaba Mselemu, amesema Issa alitumia miaka mitatu akiwa gerezani kupata mafunzo ya ushonaji yaliyotolewa kwa ushirikiano na Chuo cha VETA Kihonda Morogoro. Amesema mafunzo hayo yamekuwa na umuhimu mkubwa katika kuwaandaa wafungwa kwa maisha ya nje ya gereza, kwa kuwapatia ujuzi unaoweza kuwasaidia kujiajiri.


Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Kihonda, Fred Uriki, amesema chuo hicho kimeanzisha ushirikiano na Jeshi la Magereza kwa lengo la kuwafundisha wafungwa katika fani mbalimbali za ufundi. Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wafungwa wanapomaliza vifungo vyao kutumia ujuzi walioupata kujiajiri, kuanzisha shughuli za uzalishaji na kujipatia kipato.


Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Magereza (SACP) Peter Anatory, amesema kazi ya Jeshi la Magereza si kuwahifadhi wafungwa pekee, bali pia ni kuwasaidia kurekebika na kuwaandaa kurejea katika jamii wakiwa watu bora. 


Amesema kuwapatia mafunzo ya ujuzi ni moja ya njia zinazosaidia kuwajengea uwezo wa kuishi maisha ya kawaida na kufanya shughuli halali baada ya kumaliza vifungo vyao.


Issa Mohamed Kitambi amelishukuru Jeshi la Magereza kwa kumpatia fursa ya kujifunza ushonaji pamoja na The Islamic Foundation kwa kumpatia cherehani hiyo na kusema kuwa, msaada huo utamsaidia kuendeleza taaluma aliyojifunza akiwa gerezani na kuwa chanzo cha kipato katika maisha yake mapya, huku akiahidi kutumia fursa hiyo kwa manufaa yake na jamii kwa ujumla.






Comments

Popular posts from this blog

RAIS SAMIA AKIPEWA POLE NA VIONGOZI MBALIMBALI

SHULE YA MSINGI IPULI YAPEWA TUZO YA UFANISI

MRADI WA BOMBA LA MAFUTA KUANZA JANUARI 2027

TARURA YATENGA BIL. 1 KUKABILIANA NA EL NINO TABORA

MAKAMU WA RAIS AMWAKILISHA RAIS DKT. SAMIA SULUHU HASSAN, UTOAJI WA TUZO ZA PYMA.

MAONESHO YA MADINI YAIPAISHA LINDI KIMAPATO - MAKUSANYO YAFIKIA BILIONI 10.5

MBEYA DC YAPOKEA MRADI KUHIFADHI MAZINGIRA BONDE LA MTO SONGWE

MWENYEKITI MBEYA DC ASHIRIKIANA NA WANANCHI KUCHIMBA MSINGI WA SHULE