Saturday, May 11, 2024

MLAO AWAASA MADIWANI MKOA WA PWANI.

 

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani Mwishehe Mlao akizungumza na Madiwani hao (Hawapo pichani) Picha na Omary Mngindo.

...................................

Na Omary Mngindo, Pwani.

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao, amekutana na Madiwani kutoka katika Halmashauri zote zinazounda mkoa wa Pwani, lengo ni kutathmini kuelekea uchaguzi ujao.


Katika kikao hicho kilichofanyika wilayani Mkuranga, Mlao amewaagiza madiwani hao  kuhakikisha chama hicho kinashinda kwa kishindo katika chaguzi za Serikali za mitaa, Vijiji na Vitongoji kwa mwaka 2024.


Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti huyo akiwakumbusha kuzingatia maadili, kuepuka udini, kutumia mitandao ya kijamii kwa tija, ukaribu na wananchi wakiwemo wana CCM kuelezea mazuri yanayofanywa na Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu.


"Yeyote atakaye kiuka maadili ya chama chetu kwa kutukana mitandaoni, ninaagiza kuanzia sasa aitwe katika vikao husika na kujadiliwa sanjali na kuchukuliwa hatua za kinidhamu" alisema Mlao.


Aidha amewasisitizia madiwani hao pamoja na wanaCCM kuacha mara moja kujichukulia dhamana ya kuwa wasemaji katika mitandao au vijiwe bila kuwa na uhalali huo.


Kwa upande wake Katibu wa chama hicho mkoani hapa Bernard Ghaty alitumia nafasi hiyo kuwatahadharisha madiwani hao, akiwataka kuhakikisha hawapotezi  mitaa, viijiji wala vitongoji katika kata zao.


"Lengo la chama chetu ni kuhakikisha mitaa, vijiji na vitongoji vyote vinarudi CCM, mkumbuke Mwenyekiti wetu alipokea kijiti hiki nafasi zote za uongozi zikiwa CCM, ndoto yake ni kuona vijiji vyote vinarudi,' alisema Ghaty.


"Madiwani wa viti maalum fanyeni ziara kwenye Halmashauri zenu na si katika kata mnazoishi, nendeni mkakiimarishe chama, shughulikieni masuala yote pia kuzisimamia kwa mujibu wa sheria na kanuni katika majukumu yenu," alisisitiza Ghaty.


Aidha Katibu huyo amehitimisha kwa kuwataka Madiwani hao kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024, kwa kuhakikisha wanatatua changamoto zinazowakabili wananchi ili chama hicho kiweze kushinda kwa asilimia zote.


Katika kikao hicho Madiwani hao wameahidi kwenda kutekeleza maagizo yaliyotolewa, na kwamba watafanya kazi kwa bidii na uzalendo ikiwa ni kuendelea kumuunga mkono Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa.





No comments:

Post a Comment