Tuesday, May 28, 2024

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU KITAIFA 2024 AWAPA HEKO MTAMA KWA KUANZISHA KITUO CHA REDIO

 

Na HADIJA OMARY, LINDI


kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2024 Godfrey Mnzava ameipongeza halmashauri ya Mtama Mkoani Lindi kwa uibuaji wa mradi wa  kituo cha kurusha matangazo cha Redio Mtama.


Mradi huo wa ujenzi wa studio za redio jamii Mtama FM(106.3) uliibuliwa mwaka 2023 chini ya ufadhili wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) uliopo chini ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.



Akizungumza na wananchi mara baada ya mwenge wa uhuru kutembelea katika Redio hiyo iliyopo katika Mtaa wa majengo katika halmashauri hiyo  kiongozi huyo amesema mradi huo ni mzuri na kwamba utawezesha halmashauri kufikisha Taarifa kwa wananchi kwa uharaka.



Hata hivyo Mnzava ameitaka  jamii kutumia kituo hicho ili kiweze kuleta tija kwao na kutoa wito kwa uongozi wa halmashauri kukamilisha ujenzi wa kituo hicho kwa hatua zilizobaki ili kiweze kuanza kutumika kwa wakati.


Aidha Mnzava ametumia fursa hiyo kueleza umuhimu wa vyombo vya habari na kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru 2024 ambayo inasisitiza juu ya Umuhimu wa kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Utunzaji wa Mazingira.


Akitoa taarifa kwa kiongozi wa Mbio za Mwenge Mhandisi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF ) Mhandisi Baraka Elieza amesema mradi huo  unatekelezwa na makandarasi ElsewedyElectric East Africa Ltd P.O BOX 9213 DSM ukiwa na gharama kiasi cha Tsh. Milioni 972 huku gharama zote zikilipwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote yaani UCSAF.



Mhandisi Elieza ametaja wanufaika wa mradi huo kuwa ni wananchi wote kutokana na redio hiyo kusikika kwenye kata zote 20 za Halmashauri ya Mtama, kutumia redio katika kuelimisha jamii kupitia vipindi mbalimbali, kutumia redio kama chanzo cha mapato ya halmashauri kutokana na kurusha matangazo ya wateja mbalimbali.





No comments:

Post a Comment