Monday, May 27, 2024

LUGANGIRA KUANZISHA MABINT CUP KAGERA.

 

Mbunge viti maalum (CCM) mkoa wa Kagera Neema Lugangira akizumgumza na waandishi wa habari hawako pichani

.........................

Na Alodia Babara,  Bukoba

Mbunge viti maalum (CCM) mkoani Kagera Neema Lugangira ameanza maandalizi ya ligi ya mpira wa miguu  maarufu kama Mabintcup itakayowahusisha watoto wa kike na wanawake.


Maandalizi ya ligi hiyo tayari yameanza kwa kuunda kamati tendaji ambayo wajumbe wa kamati hiyo ni pamoja na Katibu wa chama cha soka mkoa wa Kagera Alhaji Amir, mkurugenzi wa Bukoba tour Wiliam Ruta, mwenyekiti wa chama cha soka wanawake mkoa wa Kagera Dkt Leonia Kaijage, mtu wa habari za mitandaoni na yeye mbunge Lugangira akiwa ni mwenyekiti wa kamati hiyo ambayo itashirikiana na watu wengine.

                   

Neema Lugangira mbunge viti maalum mkoani Kagera jana akizungumza na waandishi wa habari mjini Bukoba ambao wamejiunga pamoja kwa hiyari yao kuunga mkono agenda ya Mabinti Cup ametaja malengo ya kuanzisha ligi hiyo kuwa ni kuunga mkono juhudi za Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuhamasisha usawa wa kijinsia.


Malengo mengine ni pamoja na kutumia michezo kama nyenzo ya kuchagiza maendeleo kwa kuimarisha demokrasia na maendeleo, fursa za kiuchumi, afya ya uzazi kwa wanawake, vijana wa kike na kiume.


Rugangira amesema Mabinti Cup anaianzisha kama yeye kwa kushirikiana na chama cha soka mkoa wa Kagera KRFA si kwa matakwa ya kisiasa bali kwa mapenzi aliyonayo katika soka.


“Baada ya kutafuta timu zitakazoshiriki kwenye ligi kadiri mechi zitakavyokuwa zinaendelea vitaibuliwa vipaji na kuvitambua ili vikuzwe, kwenye kuibua na kukuza vipaji hapo tutajitahidi kutafuta timu kubwa za wanawake ili mashindano yawe ni kama  kiwanda cha kuzalisha vipaji” amesema Lugangira.


Ameongeza kuwa, viwanja vitakavyotumika kwenye michezo vitafanywa kama kambi  ya elimu ili kupitia michezo yahamasishwe maendeleo.


“Kama mechi inaanza saa 10:00 masaa mawili kabla yatatumika kutoa elimu juu ya maswala mbalimbali ambayo ndiyo malengo yetu na kaulimbiu ya Mabinti Cup ni piga kete ukatili wa kijinsia” amesema Lugangira.


Ligi hiyo inatarajia kuanza Novemba mwaka huu wachezaji ni vijana kuanzia miaka 18 hadi 25 timu zitakazoshiriki ni 16 huku timu 14 zikiwa za manispaa ya Bukoba, timu moja kutoka wilaya ya Misenyi na nyingine moja kutoka Bukoba Vijijini ambazo zitacheza kwa njia ya mtoano.


Aidha Lugangira amesema kuanzia mwezi June hadi Julai watasajili timu na kupata viongozi, Agosti zitatolewa semina kwa wachezaji na viongozi na kuanzia Septemba hadi Oktoba ni mazoezi kwa timu zitakazokuwa zimepatikana.


Amesema ligi hiyo itakuwa ni mwendelezo kutoka ngazi ya wilaya, mkoa, kikanda hadi Taifa.


Faisal Hamed ni mwandishi wa habari kutoka kituo cha Eatv amemshauri mbunge huyo kuwa, watakapokuwa wanatafutwa wachezaji wa kushiriki katika ligi hiyo kamati ipite na kwenye vituo vya watoto yatima kwani huko wanaweza kupatikana wachezaji bora.


Ameeleza kuwa, kutokana na kwamba wakati ligi inaendelea wanahitaji kuibua vipaji vya mabinti basi kamati ipite kwenye vituo hivyo ili kuweza kuibua vipaji kwani michezo hiyo inaweza kuwa faraja kwa mabinti wanaolelewa katika vituo vya watoto yatima.


Diana Deus mwandishi wa habari gazeti la Habari Leo amemshukuru mbunge kwa wazo la kuanzisha ligi hiyo na kusema kuwa ligi hiyo itasaidia kuibua vipaji kwa vijana wa kike na ili kuweza kutimiza kauli mbiu ya ligi hiyo na waandishi wa habari kuandika kwa undani zaidi habari za unyanyasaji wa kijinsia akaomba mafunzo kwa waandishi hao.


No comments:

Post a Comment