Friday, May 24, 2024

UMARUKI WATUMIA MILIONI 7, KUSAIDIA WAATHIRIKA WA MAFURIKO PWANI.

 


Viongozi wa Umoja wa Maendeleo wa Watu wa Rufiji mkoani Pwani na Kilwa mkoani Lindi (UMARUKI) waishio Morogoro, wakikabidhi msaada huo kwa Mkuu wa mkoa wa Pwani ambao umepokelewa na Katibu tawala mkoani Pwani (RAS)  Rashid Mchata kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo.

....................................

Na Rashid Mtagaluka, Kibaha.


Umoja wa Maendeleo wa Watu wa Rufiji mkoani Pwani na Kilwa mkoani Lindi (UMARUKI) waishio Morogoro, jana Mei 23/2024 umekabidhi msaada wa nguo kwa wananchi waliopatwa na athari ya mafuriko mkoani Pwani.


Akizungumza wakati akikabidhi msaada huo kwenye ofisi za Mkuu wa mkoa wa Pwani, Katibu Mkuu wa UMARUKI Bwana Juma Mtumbei alisema umoja huo umeguswa na tukio hilo, hivyo kama binadamu wameona wanao wajibu wa kuwasaidia.


Kwa mujibu wa Mtumbei, msaada waliotoa kwa waathirika hao ni pamoja na nguo za watoto, wanawake, wanaume pamoja na nguo maalumu za kujistiri wakati wa baridi zote zikiwa na  thamani ya shilingi Milioni Saba na laki saba.


Kwa upande wa Katibu tawala mkoani Pwani Rashid Mchata aliyepokea msaada huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, amewashukuru UMARUKI kwa moyo wao  wa kujitolea kuwasaidia wananchi wa wilaya za Rufiji na Kibiti zilizokumbwa na athari za mafuriko.


Mchata ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa taasisi nyingine za kiraia kufuata nyayo za UMARUKI kwa kuona umuhimu wa kuisaidia serikali katika jukumu la kujitolea kwa watu waliopatwa na majanga kama hao wa mkoani Pwani.


Naye Naibu Katibu Mkuu wa Umoja huo Mwalimu Habib Salim Muhinge ameishukuru ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Pwani kwa kukubali kwao kupokea mchango wao huo ingawa ni mdogo lakini ofisi hiyo haikuona tabu kuupokea.


Aidha Muhinge amewashukuru wanajumuiya ya UMARUKI waishio Morogoro na kuwataka wasiishie hapo tu, bali moyo huo wa kujitolea wauendeleze kila inapotokea watu kuhitaji msaada popote pale nchini.


Salha Mbonde ambaye ni miongoni mwa wajumbe wa UMARUKI aliyeongozana na viongozi kupeleka msaada huo Mkoani Pwani, amewaomba kina mama kote nchini kutumia fursa hii kuona umuhimu wa kuisaidia jamii kila inapoonekana kuna haja ya kufanya hivyo.


Umaruki ni asasi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa na wananchi wa mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara waishio Morogoro kwa lengo la kusaidiana, na  ambayo imesajiliwa serikalini kwa namba S.A.19402.


No comments:

Post a Comment