Na Omary Mngindo, Kisarawe
MWENYEKITI wa Jumuia ya Wazazi Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani Khamis Dibibi, mwishoni mwa wiki amegawa vitendeakazi kwa viongozi wa matawi 119 yaliyopo Kata zote 17 wilayani hapa.
Katika hafla hiyo chini ya mgeni mualikwa Kaimu Katibu wa Jumuia hiyo mkoani hapa Sophia Abdul, Dibibi alikabidhi vifaa hivyo lengo ni kuwawezesha viongozi kutekeleza shughuli za kuwatumikia wanachama.
Vifaa alivyokabidhi ni pamoja na mihuri, reja za kusajiria wanachama wapya katika matawi, vidau vya mihuri (Stap Pad), kadi za Jumuiya ya wazazi 300 kila tawi sanjali na bips (Reflector).
"WanaJumuia wenzangu nimeamua kununua vitendeakazi hivi, lengo kubwa kuwawezesha katika kutekeleza majukumu yetu ya Jumuia, pia niwaombe tuhamasishe wanachama wapya wajiunge," alisema Dibibi.
Akizungumza na wanaJumuia hao, mgeni mualikwa amehimiza umoja, mshikamano na upendo huku akiwataka kujitokeza kuwania nafasi ya Wenyeviti wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.
"Tumpongeze Mwenyekiti wetu Khamis Dibibi kwa kutuwezesha vitendeakazi hivi, niwaombe tukavitumie katika kuhakikisha vinatusaidia kuwatumikia wanaJumuia," alisema Sophia.
Aidha aliongeza kwamba "Twendeni tukahamasishe wanachama wapya wajiunge katika Jumuia yetu, pia tugombee uenyekiti wa serikali katika uchaguzi ujao," alimalizia Kaimu Katibu huyo.
No comments:
Post a Comment