Na Hadija Omary, Lindi
Zaidi ya watu 6,000 wa vijiji vya Chiuta, Mikongi na maeneo ya jirani katika halmashauri ya Mtama Mkoani Lindi wameanza kunufaika na upatikanaji wa huduma ya uhakika ya maji safi na salama.
Hiyo ni baada ya kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Kitaifa kwa mwaka 2024 Godfrey Mzava kuweka jiwe la msingi katika mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya maji Chiuta -Mikongi, Mei 27,2024.
Mradi huo unaogharimu Kiasi cha zaidi ya Milioni 452 umeboreshwa kwa lengo la kukidhi mahitaji halisi ya wananchi wa vijiji vya Chiuta na Mikongi ambapo hapo awali ulikuwa unatoa huduma ya maji chini ya asilimia 30 ya mahitaji halisi kwa jamii ya Kijiji cha Chiuta Pekee.
Akitoa taarifa ya mradi mbele ya kiongozi wa mbio za mwenge Kitaifa, Mhandisi wa mradi huo Olaph John amesema mradi huo unatekelezwa na Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Masasi kwa kushirikiana na Shirika la World Vision kwa usimamizi wa Serikali kupitia wakala wa maji safi na usafi wa mazingira Vijijini (RUWASA) ambapo kwa uboreshaji huo unakwenda kutoa uhakika wa upatikanaji wa maji kwa wananchi Kwani utazalisha maji takribani lita 168,000 kwa siku badala ya Lita 7,490 zilizokuwa zinazalishwa hapo awali.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za mwenge Kitaifa kwa mwaka 2024 Mnzava amelishukuru Kanisa la Anglikan kwa namna linavyoiunga Mkono Serikali katika kuwahudumia wananchi akiwataka pia kumaliza shughuli zilizosalia katika mradi huo huku wananchi wa Chiuta wakiahidi kutunza miundombinu yake.
Mradi wa uboreshaji wa maji Chiuta -Mikongi utatumia mfumo wa malipo ya kabla (Pre -Paid Meters)kwenye vituo vyake vyote vya kuchotea maji.
No comments:
Post a Comment