Saturday, May 11, 2024

MTU MMOJA AFARIKI KWA KUSOMBWA NA MAJI BUKOBA.

 

Na Alodia Babara, Bukoba

Mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha kifo cha mtu mmoja katika kata ya Bakoba manispaa ya Bukoba mkoani Kagera huku barabara zikifungwa kwa muda kutokana na baadhi ya madaraja katika barabara hizo kufunikwa na maji.


Kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoani Kagera Zabron Muhumha akizungumza leo ametaja aliyefariki kwa jina moja la Lea anayekadiliwa kuwa na umri wa miaka 19 ambaye wakati anachota maji mtoni aliteleza na kusombwa na maji ya mvua.


"Mei 09,2024 majira ya saa 4:00 jioni binti huyo akiwa anachota maji katika mto aliteleza na kusombwa na maji na mwili wake ulipatikana  na kupelekwa kuhifadhiwa hospitali ya Rufaa ya mkoa, Bukoba" alisema Muhumha.


Ametaja madhara mengine yaliyopatikana na mvua hizo kuwa zimesababisha nyumba nyingi ambazo ziko mwambao wa mto Kanoni na ziwa Victoria kuzingirwa na maji na baadhi ya barabara kufungwa kwa muda.


Ametaja maeneo ambayo yamezingirwa na maji kuwa ni Kiwanja cha Jymkana kata ya Miembeni, baadhi ya nyumba Kasalani na Nyakanyasi kata ya Bakoba, Nyamkazi kata ya Miembeni na  Omukigusha  kata ya Bilele.


Aidha amesema jeshi hilo linaendelea kutoa elimu na linazungukia maeneo ambayo ni hatarishi na kuwajuza wananchi wahame maeneo hayo, kila mwaka yamekuwa yakijaa maji kwa kuwa mvua zinaendelea kunyesha ardhi imejaa maji hata ikinyesha mvua ya wastani maji yanajaa mengi sana hivyo wahamie maeneo salama.


Kwa upande wake Diwani wa kata ya Bakoba Shaaban Rashid amesema kuwa, katika kata yake mtaa wa Nyakanyasi eneo la Mwizinga mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia Mei 10,2024 ilisababisha eneo hilo kujaa maji na walikuwa wanaendelea na zoezi la kutoa watu ndani ya nyumba na kuwapeleka maeneo salama.


Amewaomba wananchi ambao maeneo yao huwa yanajaa maji hata kama bado hayajawafikia kuhama maeneo hayo kwa ajili ya kulinda usalama wao.


Aidha diwani wa kata ya Miembeni
Richard Gaspal amesema kuwa katika mtaa wa Nyamkazi eneo hilo limejaa maji kwani ni eneo ambalo liko mwambao wa ziwa Victoria na hata barabara hazipitiki zimejaa maji  na daraja lililojengwa hivi karibuni limefunikwa na  maji hivyo wananchi wanapita kwenye vichochoro wanapanga mawe wanapita ili kuhama katika maeneo yao na kwenda maeneo salama.


Amesema, baadhi ya waathirika wamehamia kata ya Kashai na wengine wamewawekwa sehemu moja katika shule ya msingi Nyamkazi.


Ikumbukwe kuwa, mji wa Bukoba ni mji ambao uko katika mwambao wa ziwa Victoria na kuna mito inapita katika mji huo ikimwaga maji yake katika ziwa hilo na nyumba zaidi ya 70 zimeathiriwa na maji.


No comments:

Post a Comment