Wednesday, May 29, 2024

KLABU ZA WAPINGA RUSHWA MASHULENI ZINASAIDIA KUENDELEZA  MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA

 

Na Hadija Omary, Lindi.


Imeelezwa kuwa Kuanzishwa kwa klabu za wapinga rushwa mashuleni ni chachu ya kuimarisha na kuhamasisha wanafunzi kupenda kushiriki kwenye vitendo vya kuzuia, kupinga na kupambana na rushwa katika jamii.


Hayo yameelezwa na  Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024,  Godfrey  Mnzava alipotembelea Klabu ya Wapinga Rushwa ya Shule ya Sekondari Hawa Mchopa iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Mkoani Lindi. Kwa lengo la kuimarisha klabu hiyo.


Mnzava  amesema kuwa kwa kuzingatia kauli mbiu ya KUZUIA RUSHWA NIJUKUMU LAKO NA LANGU, TUTIMIZE WAJIBU WETU,  jamii inapaswa kuendelea kutoa msisitizo na kuwekeza zaidi katika kuelimisha wanafunzi ambao ndio viongozi wa kesho ili waweze kujua madhara ya Rushwa kwa jamii.


"Tuweke nguvu zaidi katika kuunda klabu za wapinga rushwa mashuleni na vyuoni ili kuwaandaa hawa viongozi wetu wa kesho kujua madhara ya rushwa na kuichukua rushwa ili tuweze kujenga taifa la watu wanaoichukia rushwa na kutoa haki vile inavyopaswa" ameeleza.


Awali akitoa taarifa ya Klabu ya Kuzuia na Kupinga Rushwa, Katibu wa Klabu hiyo Noshard Christopher ameeleza kuwa kupitia Klabu hiyo wanafunzi wamepata fursa ya kutambua madhara na viashiria vya rushwa pamoja na kuelimisha wanajamii kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa kupitia nyimbo, ngonjera, uchoraji wa katuni na uandishi wa insha.


"Tuna imani kwamba uwepo wa vilabu vya kupinga Rushwa mashuleni na vyuoni vinasaidia jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya Rushwa na hivyo kujenga Tanzania imara isiyokuwa na Rushwa.


Vilevile, tunawahamasisha wananchi kufichua na kukemea vitendo vya Rushwa katika maeneo yao kwa kutoa taarifa ofisi ya TAKUKURU kwa njia ya simu namba ya  bure 113" ameongeza Noshard.


Amesema klabu ya Wapinga Rushwa katika Shule ya Sekondari Hawa Mchopa ilianzishwa miaka 7 na hadi sasa jumla ya wanachama hai 122, kati yao wavulana ni 71 na wasichana 51.




No comments:

Post a Comment