Na Alodia Babara,
Bukoba
Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa ametaja manufaa manne yatakayopatikana baada ya kukamilika ujenzi wa tawi la chuo kikuu cha Dar es Salaam ikiwemo kupanua mji, kukuza uchumi, kuongeza fursa kwa vijana wa Kagera na kuongeza urafiki.
Tawi hilo la chuo kikuu litajengwa katika kijiji cha Itahwa kata ya Kalabagaine halmashauri ya Bukoba na eneo la chuo hicho ni hekali 315 ambazo zilitolewa na wananchi wa vijiji viwili vya Kangabusharo na Itahwa na hafla ya kukabidhi eneo la ujenzi kwa mkandarasi imefanyika Mei 29,mwaka huu.
Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa akiwa mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika katika eneo litakapojengwa tawi la chuo kikuu cha Dar es Salaam amewashukuru wananchi kwa kutoa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho na kutoa manufaa manne yatakayopatikana baada ya kukamilika kwake.
"Nitumie nafasi hii kumshukuru Rais wa Jamhuli ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutukumbuka wanakagera kutuletea fedha kwa ajili ya ujenzi wa chuo kikuu, wanakagera walitamani kuwa na chuo kikuu miaka mingi iliyopita kwani wanahistoria ya kupenda kusoma" amesema Mwassa
Ameongeza kuwa, wanatambua chuo hicho ni kwa ajili ya watanzania wote na raia wa nchi nyingine lakini watatumia fursa hiyo vizuri.
Amesema kuwa, uwepo wa mradi huo utaleta fursa mbalimbali kwa wakazi wa mkoa wa Kagera ikiwemo fursa ya elimu kwa wakazi wa Kagera kwani kitakuwepo kituo cha mafunzo ya ujasiriamali hata kama mtu hajamaliza kidato cha sita, kupanua mji, kukuza uchumi, na kuongeza urafiki.
Aidha ametoa rai kwa wanafunzi wanaosoma shule za sekondari zinazozunguka eneo la chuo kikuu kuongeza bidii katika masomo ili watakapohitimu kidato cha sita waweze kuendelea na masomo ya juu katika chuo hicho.
Pia amemtaka mkandarasi wa ujenzi katika chuo hicho kumaliza kwa wakati ujenzi huo.
Kwa upande wake Naibu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayeshughulikia taaluma Prof. Beneventura Rutinwa amesema mpango wa ujenzi wa tawi la chuo hicho ulianza mwaka 2019 na kwa kipindi cha kwanza cha ujenzi zitatumika shilingi bilioni 20.
Amesema ujenzi ulianza Mei 17,2024 utakamilika Octoba mwaka kesho utachukua muda wa miezi 18.
Aidha mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Sima amesema, wilaya ipo tayari kutoa ushirikiano kipindi chote cha utekelezaji wa ujenzi huo.
No comments:
Post a Comment