Tuesday, May 21, 2024

JKT RUVU WAUNGA MKONO JUHUDI ZA RAIS SAMIA SEKTA YA UTALII.

 

Kanali Peter Mnyani (Mwenye suti) na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John wakifunua kitambaa kuashiria kuzinduliwa kwa zuu hiyo. Picha na Omary Mngindo.

....................................

Na Omary Mngindo, Ruvu.

JESHI kambi ya Ruvu JKT iliyopo Mlandizi Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani, imeunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Saluhu katika suala la kutangaza vivutio mbalimbali vilivyopo vikiwemo vya wanyamapori kupitia sekta ya utalii.

Hatua hiyo inatokana na kambi ya Ruvu kuanzisha kitalu cha kuhifadhia wanyama hao, kwa kutenga ardhi yenye ukubwa wa eka 70, pembezoni mwa kambi wakianza na Twiga, Swala, Pundamilia na wengine wadogowadogo.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Kikosi hicho Kanali Peter Mnyani, mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John, wakati wa uzinduzi wa zuu hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wanajeshi wastaafu na mamia ya wananchi.

"Mkuu wa Wilaya uanzishwaji wa zuu ya wanyama tunalenga kuunga mkono juhudi za Rais wetu Dkt. Samia Suluhu, ambae amedhamiria kuifungua nchi katika sekta mbalimbali pia tunakumbuka alizindua filamu ya Royal Tour iliyochangia kupatikana kwa watalii wengi," alisema Mnyani.

Kanali Mnyani aliongeza kuwa "Mwezi wa sita tunataraji kuleta Simba, ambae hatokuwa na madhara kwa wanamchi watakaokuja kuangalia wamyama hapa katika kambi yetu ya Ruvu," alisena Kanali huyo.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kibaha Nickson John, alipongeza ubunifu huo unaolenga kuwawezesha wananchi wa Kibaha na maeneo mbalimbali kufika kujionea wanyama hao, ambao wengine huwangalia kupitia TV.

"Uwepo wa zuu hii utasaidia wana Kibaha, lakini si wao tu ukizingatia ipo mita chache kutoka barabara Kuu ya Dar es Salaam kuelekea mikoani, hapa abiria wanaopita eneo hili wanaweza kuja kuangalia wanyama hawa," alisema Mkuu huyo wa wilaya.

Wakazi Athumani Semsega na Zainabu Issa wameelezea kufurahishwa kwao kufuatia ubunifu huo, huku wakisema kuwa umesaidia kuwaona wanyama hao kwa karibu ambapo pia waliweza kuwalisha chakula.

Kanali Peter Mnyani akimuonesha Mkuu wa Wilaya ya Kibaha,  Nickson John eneo litakalokuwa linapatikana vinywaji. 
Picha na Omary Mngindo.

Mkuu wa Wilaya Nickson John akimlisha chakula mmoja wa Pundamilia wanaopatikana katika zuu hilo. Picha na Omary Mngindo.


No comments:

Post a Comment