Na Alodia Babara, Bukoba
Mwakilishi wa mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Bukoba BUWASA mhandisi Matage Doto amesema mamlaka hiyo iko tayari kushirikiana na wadau wengine kusaidia chama cha waandishi wa habari mkoa wa Kagera (KPC) katika ujenzi wa ofisi ya chama hicho.
Hayo yamekuja baada ya mwenyekiti wa club ya waandishi wa habari mkoani hapa Mbeki Mbeki, kumuomba mgeni rasmi kutoa msaada katika ujenzi wa ofisi ya waandishi wa habari kutokana na club hiyo kuwa na kiwanja ambacho tayari kimeishapata hati miliki.
Mhandisi Doto wakati akihutubia waandishi hao Mei 15,2024 wakati akiwa mgeni rasmi kwa niamba ya Mkurugenzi wa BUWASA katika maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari yaliyofanyika kimkoa mjini Bukoba ametoa pongezi kwa club hiyo kwa mawazo ya ujenzi wa ofisi na kusema kuwa, endapo club hiyo itaanza ujenzi ishirikishe wadau mbalimbali ikiwemo mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Bukoba (BUWASA.)
“Niwapongeze kwa kuwa na mawazo ya kuwa na ofisi yenu, mtakapoandaa mchanganuo wa bajeti ya ujenzi wa ofisi yenu pamoja na kubainisha taasisi zilizopo mkoa wa Kagera kwa ajili ya kuwapa msaada na pale mtakapoona kwamba na sisi BUWASA tunaweza kusaidia tutakuwa tayari” amesema Mhandisi Doto
Aidha, akizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu inayosema uandishi wa habari na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi amesema waandishi wanapaswa kubobea katika kuandika habari Fulani ili waweze kuingia kwa undani juu ya makala wanazokuwa wanaandika.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Club ya waandishi wa habari mkoa wa Kagera Mbeki Mbeki amesema kuwa, maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari mwaka huu ni ya 31, na kutokana na takwimu kutoka World Press Freedom 2024 zimeonyesha Tanzania kufanya vizuri katika kuheshimu uhuru wa habari kwa kushika nafasi ya 97 kwa mwaka 2024 kutoka nafasi ya 142 kwa mwaka 2023.
Amesema Tanzania imepanda kwa kasi kwa nafasi 46 na kuziacha nchi nyingine za ukanda wa Afrika mashariki nyuma.
Mathias Byabato ni mwandishi wa habari mkoani Kagera akichangia juu ya kauli mbiu ya mwaka huu amesema kuwa, licha ya waandishi wa habari kuwa na wajibu wa kuelimisha jamii juu ya changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia ya nchi pia wataalamu wa mazingira kutoka serikalini wanao wajibu wa kulinda maeneo ya vyanzo vya maji kwa kusimamia sheria.
Byabato ametolea mfano wa eneo la Kasalani na Rwamishenyi manispaa ya Bukoba ambalo ni eneo la maji ya mto Kanoni lakini kimemwagwa kifusi kikionyesha kuna mtu anahitaji kufanya ujenzi katika eneo hilo.
Ikumbukwe kuwa, siku ya uhuru wa vyombo vya habari huadhimishwa kimataifa kila mwaka Mei 3 na mwaka huu imeadhimishwa Kitaifa jijini Dodoma kwa kusimamiwa na Muunganiko wa Umoja wa Vilabu nchini UTPC na mgeni rasmi alikuwa Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kasimu Majaliwa na Kimataifa iliadhimishwa nchini Ghana na baada ya siku yenyewe yameadhimishwa ngazi ya mkoa.
No comments:
Post a Comment