Sunday, May 26, 2024

WAKAZI WA MASAKI KISARAWE  WALILIA BARABARA

Na Omary Mngindo, Kisarawe

WAKAZI wa Vijiji vinavyounda Kata ya Masaki Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani, wameiomba Serikali kuandaa utaratibu wa Daladala nyingine zipitie barabara ya Kisanga kutokea Masaki.


Wakizungumza na Mwandishi wa habari hizi kijijini Masaki wakazi Fatuma Swaiba, Juma Idd na Ramadhani Seif walisema kuwa kwa sasa usafiri unaotokea Chanika bodaboda nauli ni shilingi elfu tano.


"Nauli yake kutoka Chanika mpaka kuanzia Kijiji cha Kisanga ni shilingi elfu 5,000 na kuendelea kutokana na umbali, lakini kuna umbali wa dakika 30 lakini upande wa barabara iko vizuri ukiachilia baadhi ya changamoto za maeneo machache," alisema Fatuma.


Aliongeza kuwa kwa kutumia mabasi yanayotokea stendi ya mabasi ya Pugu kuelekea Kisarawe mjini na vijiji mbalimbali wanatozwa shilingi elfu 4,000,  hivyo wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kupatikana kwa usafiri.


"Kuna abiria wengine wanatokea maeneo ya Mkuranga na vitongoji vyake ambao kwanza wanafika pale Chanika, kisha wanapanda bodaboda kuelekea vijiji na vitongoji mpaka Masaki na kuendelea vijiji vingine," alisema mkazi huyo.


Seif alisema kuwa kwa kutumia pikipiki wanazozipanda kutokea Chanika kupitia Kisanga kutokea Masaki ni mwendo wa dakika 25 mpaka 27, huku wakilipa shilingi 5,000 kwa mtu mmoja wakiwa wawili wanatozwa shilingi 6,000.


"Hii barabara ni fupi sana, itakuwa ni vema wakapitisha daladala ili kuwahakikishia kuwa na usafiri wenye uhakika tofauti na bodaboda, kwa sasa tunawashukuru kwa kazi waliyotufanyia kwa miaka mingi, sasa tunaomba dalada," alisema Seif.


Idd alisema kuwa usafiri wa mabasi kutoka Pungu kupita Kisarawe na vitongoji vingine mpaka kufika Masaki nauli yake sh. 4,000, lakini kuna mzunguko mkubwa vyombo hivyo hutumia zaidi ya masaa mawili hali inayowachosha. 






No comments:

Post a Comment