Na Omary Mngindo, Chalinze.
JUMUIA ya Wazazi Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, imeitaka Idara ya Ardhi halmashauri ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo mkoani hapa kusitisha upimaji wa ardhi katika eneo linalomilikiwa na Jumuia hiyo.
Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Jumuia hiyo Aboubakary Mlawa, katika kikao kilichojumuisha wanachama wa Jumuia kwenye kuelekea sherehe za Wazazi Kitaifa, itayotanguliwa na ya Mkoa ambapo kiwilaya imefanyika Kata ya Bwilingu.
Alisema kuwa eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 50, Jumuiya hiyo ilipewa na uongozi wa Kijiji mwaka 2000 kwaajili ya kujenga shule ya wazazi, lakini wavamizi wametoa alama za mipaka ya eneo hilo na kujenga na sasa wanarasimisha rasmi ili wapatiwe hati.
"Ardhi ni yetu hivyo kuwabana wale ambao wameingia watalazimika kutulipa hela yetu kulingana na thamani ya ardhi ya sasa, hatutawanyang'anya ila watafidia maeneo yetu kulingana na thamani ya sasa," alisema Mlawa.
Aliongeza kwamba "Mimi msimammo wangu ni huo zoezi lisimame kwa wale waliochukua mali zetu waturudishie, uzuri ni kwamba tunajua eneo letu lina ukubwa gani na linaanzia wapi," alisema Mwenyekiti huyo.
Kwa upande wake Diwani Wa Kata ya Bwililingu Nasser Karama alithibitisha kuwepo kwa eneo hilo ambalo kwa kiasi kikubwa limevamiwa na watu baadhi huku baadhi yao wakiwa wamejenga na wengine kuuza.
"Leo itanibidi niongee ukweli, moja ya vitu vinavyofanya nichukiwe na baadhi ya wananchi ni namna ninavyotetea mali za chama na serikali, ninapofanya hivyo naambiwa naleta wawekezaji, lakini nashukuru wengi wameelewa sasa baada ya watu kuona ukweli," alisema Karama.
Mwenyekiti Mstaafu wa Jumuia hiyo wakati huo ikitambulika Kata ya Chalinze Mzee Kibindu ameelezea namna ardhi hiyo ilivyogawanywa kwa viongozi, huku nae akipatiwa kwa ajili ya shughuli za kilimo.
"Baada ya zoezi hilo kulikuwepo na hatua mbalimbali za kesi, na katika mchakato huo kila tulipokuwa tunakwenda tulikuwa tunashindwa, hivyo ninachojua pale hatuna eneo," alisema Kibindu huku wajumbe wakionesha kushangazwa kutokana na kauli hiyo.
Anold Mtumuyu aliyewahi kushika wadhifa mbalimbali wakati huo aliwaambia wanaJumuia hiyo kwamba akiwa kiongozi katika Kata amewahi kutembelea eneo hilo mara kadhaa, huku akisikitishwa na kauli ya Mzee Kibindu ya kwamba Jumuia haina ardhi katika eneo hilo.
"Mwenyekiti binafsi nimesikitishwa na kauli ya mzee wetu, kumbe wakati akiwa kiongozi kumbe nae alijimegea eneo lake, mimi nashauri tuanze na yeye kwani kuna mengi tutayafahamu zaidi," alisema Mtumuyu.
Wakichangia mada Alhaj Abdallah Sakasa na Amir Mramba wameelezea masikitiko yao kuhusiana na kuchukuliwa kiholela kwa ardhi ya Jumuia, huku wakishauri hatua za kisheria zichukuliwe kuwabaini wote ambao wamehusika na kuhujumu ardhi hiyo.
No comments:
Post a Comment