Sunday, May 26, 2024

MILIONI 866 KUJENGA BARABARA KM 1.2 KWA KIWANGO CHA LAMI LIWALE

 

NA  HADIJA OMARY 

LINDI.

Wananchi wa Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi wanaishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,  kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 866,659,200.40 kwa ajili ya ujenzi wa barabara kilometa 1.2  kwa kiwango cha lami katika Halmashauri hiyo.


Wametoa shukurani hizo mara baada ya mwenge wa uhuru kufika Wilayani humo na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi huo wa mradi wa barabara ambao unatajwa utarahisisha usafirishaji wa mazao.


Hamisi Rashidi, Dereva Boda boda amesema kipindi cha masika Barabara hiyo ilikuwa ikijaa maji mara kwa mara hali iliyopelekea kutopitika kwa urahisi kipindi hicho cha masika hivyo ujenzi wa barabara hiyo unaenda kumaliza kero hiyo.


Kwa mujibu wa Meneja wa wakala wa Barabara za mijini na vijijini TARURA Wilayani Liwale, Mhandisi. Living Stone Shija, amesema mradi huo wa barabara ya Murua-Mkurunguche- Ngojwike - Mandepe petrol station  unatekelezwa na mkandarasi M/S TECHINO COMBINE CONSTRUCTION  LIMITED.


Amesema mradi huo ulianza matengenezo yake tarehe 15/09/2023 na unatarajiwa kukamilika tarehe 15/07/2024 ambapo mpaka sasa tayari kazi mbalimbali zimeshafanyika.


Kwa upande wake  Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Godlack Mlinga amesema Mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Wilaya hiyo ya Liwale katika kuyafikia maeneo tofauti, kupendezesha mandhari ya mji pamoja na kupunguza adha ya matengenezo ya mara kwa mara.


" niishukuru serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya matengenezo ya Barabara hasa hizi za kati kati ya mji katika Wilaya yetu ambazo kwanza zinaenda kubadilisha muonekano wa mji wetu lakini pia kupitia bunge la bajeti serikali imeidhinisha fedha kwa ajiri ya ujenzi wa barabara ya Liwale-Nachingwea-Masasi na sasa tunasubiria kuanza utekelezaji wake"


Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika Mradi huo kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mzava  amesisitiza kuendelea kutumia mfumo wa manunuzi wa kimtandao wa Serikali wa nest.


Baada ya kukagua barabara na kukagua nyaraka zinazoonyesha uhalali wa matumizi ya fedha pamoja na utaratibu ambao umetumika katika utekelezaji wa mradi huu mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2024 umeridhia kuweka jiwe la msingi katika mradi huu.








No comments:

Post a Comment