Naibu Waziri wa Nishati,Subira Mgalu akiongea
na wananchi wa kijiji cha Matipwili kilichopo kata ya Mkange, Wilaya ya
bagamoyo, Mkoa wa Pwani alipokuwa kwenye ziara ya kazi ya ukaguzi wa kazi ya
usambazaji umeme.
..............................................
Hafsa
Omar-Pwani.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa
Huduma ya Nishati na Maji (EWURA) kuharakisha uandaaji wa kanuni ambazo
zitatumika kudhibiti bei za umeme ambazo zitatumiwa na wawekezaji binafsi wa
umeme nchini.
Ameyasema
hayo, Februari 20,2020 wakati alipokuwa akijibu maswali mbalimbali ya wananchi
ambao walikuwa wakilalamikia bei kubwa ya umeme wanaotozwa na Mkandarasi wa
kampuni ya Husk Power iliyopo katika kijiji cha Matipwili kata Mkange, Wilaya
ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.
Alisema,
Ewura inatakiwa kuyafanyia kazi maelekezo hayo kwa haraka ili wawekezaji hao
wadogo, wapate muongozo huo ambao utawasaidia kufanya kazi kwa kufuata sharia
za nchi bila ya kujichukulia maamuzi ya kujiwekea bei za juu ambazo zinawaumiza
Watanzania wa kipato cha chini.
Alifafanua
kuwa, Serikali ilitoa fursa kwa wawekezaji hao kuwapelekea umeme Watanzania
ambao wapo katika maeneo ambayo yapo mbali na gridi ya Taifa na Serikali
iliamua kutoa ruzuku ili wawekezaji hao watoe bei nafuu ya umeme kwa Watanzania
wa kipato cha chini.
“Ni
kweli wao wamewekeza miundombinu yao hapo lakini haiwezekani 5000 itumike kwa
siku, haiwezekani kabisa, pia haiwezekani laki tatu na nusu iwe bei ya mtumiaji
wa kioski kweli hiyo hapana, laki tatu na nusu ni umeme unaotumika kwenye kiwanda
cha saizi ya kati lakini sio kioski” alisema Mgalu
Alieleza
kuwa, Serikali inajukumu la kuwalinda watumiaji wa Nishati nchini, kwa
kuzingatia jukumu hilo, inawakumbusha wawekezaji nchini kuwa bei ya kunganisha
umeme vijijini ni 27000 na kuwataka wawekezaji hao kupunguza gharama za
undeshaji wa kampuni zao ili waweze kujiendeshe kwa kupata faida kwenye kampuni
zao.
“Tunataka
wapunguze gharama za uendeshaji watumie wataalamu wa ndani, watumie vifaa vya
ndani ili gharama za uendeshaji zishuke ili watanzania hawa wapate nafuu
vyenginevyo gharama za umeme zisiposhuka sisi tutakwenda hata maeneo
ambayo tulisema waende wao watakosa hii fursa kwasababu sisi hatutakubali bei
kama hizo”alisema
Aidha,alimtaka
mkandarasi huyo kukutana na Meneja wa TANESCO mkoa wa Pwani ili kujadiliana na
kuzipitia tena bei za umeme ambazo zinatumiwa na mkandarasi huyo, ili
kupatikane uwiano wa bei za umeme vijijini ambazo zinatawanufaisha
Watanzani wote ili waweze kujiletea maendeleo.
Naibu Waziri wa Nishati,Subira Mgalu
akiwasikiliza wananchi wa kijiji cha Matipwili kata ya Mkange, wilaya ya
Bagamoyo, Mkoa wa pwani alikuwa kwenye ziara ya kazi ya ukaguzi wa kazi ya
usambazaji umeme.
Mwanakijiji wa kijiji cha Matipwila kilichopo
kata ya Mkange, Wilaya ya bagamoyo, Mkoa wa Pwani akiuliza mwaswali kwa Naibu
Waziri wa Nishati,Subira Mgalu wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika
kijijini humo.
No comments:
Post a Comment