Tuesday, February 4, 2020

MASHIRIKA YA KISHERIA LINDI YALALAMIKIA TOZO KUBWA SERIKALINI.

NA HADIJA HASSAN, LINDI

WASAIDIZI WA KISHERIA Manispaa ya Lindi Mkoni humo wameiomba serikali kupunguza mrundikano wa tozo zinazotozwa katika mashirika mbali mbali ya usaidizi wa kisheria hapa nchini.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Msaada wa Kisheria Mingoyo (SHIMKIMI) Manispaa ya Lindi Mkoani humo Nuhu Mkapanda alipokuwa anazungumza na BAGAMOYO KWANZA BLOG hivi karibuni ofisini kwake.

Mkapanda alisema awamu ya kwanza mashirika hayo ya usaidizi wa Kisheria hapa Nchini yalikuwa yanasajiliwa na wizara ya Afya jinsia, wazee na watoto ambapo walikuwa wanalipa pesa elfu 50 kwa ajili ya usajili kila baada ya miaka mitatu na shilingi elfu 50 kwa ajili ya ada kila mwaka.

Mkapanda aliongeza kuwa kuanzia mwaka jana 2019 Mashirika hayo pamoja na kusajiliwa katika Wizara hiyo pia wamelazimika kusajiliwa tena kwenye Wizara ya katiba na Sheria ambapo wanatakiwa kulipia tena shilingi elfu 60 kwa ajili ya usajili wa shirika kila baada ya miaka mitatu na elfu 60 kwa ajili ya ada kila mwaka huku wasaidizi wa kisheria wakitakiwa kulipa elfu 30 kwa ajili ya usajili wa kwao binafsi pamoja na elf 30 kwa ajili ya kulipia ada.

“Hali hii inatufanya kwa upande wa Mashirika yenyewe peke yake tuanatakiwa kulipia kiasi cha shilingi 110,000 kwa ajili ya ada kwa wizara zote mbili tulizosajiliwa, na kwa mfano sisi hapa SHIMKIMI tupo wasaidizi wa Kisheria tisa ambapo tanatakiwa kulipia 270,000 sawa na jumla ni 380,000” alisema Mkapanda

“Hii inatuwia mzigo mkubwa kwetu sisi wasaidizi wa kisheria kwa sababu sisi hatulipwi mshahara kutoka sehemu yoyote kazi zetu ni zakujitolea pesa hizi tunazitoa wapi? Na ukizingatia lengo kubwa la kuanzisha mashirika haya ni kusaidia jamii hivyo endapo kama haya mashirika yatafungwa kutokana na michango mikubwa basi tujue kwamba watakaoathirika zaidi ni jamii” Alifafanua mkapanda


Kwa upande wake Victoria Mtemo Msaidizi wa kisheria kutoka katika shirika hilo la usaidizi wa kisheria mingoyo (SHIMKIMI) alisema kwamba fedha hiyo kubwa ambayo inayotumika kulipa Serikalini ingekuwa inabaki Katika mashirika yenyewe ingeweza kusaidia kupanua wigo wa kutoa elimu ya kisheria katika maeneo mbali mbali ambayo mashirika hayo hayajayafikia.

“Kwa mfano huku kwetu Lindi maswala ya Elimu ya ukatili wa kijinsia , ukatili wa watoto wanajamii walio wengi bado hawajapata kabisa na bado hawajui wapi wapeleke malalamiko yao, mathalani sasa hivi kunashida sana ya wababa kuwatelekeza watoto hasa wale wanaochepuka nje ya ndoa kuanzia mimba mpaka mtoto anapozaliwa hivyo hawa wote tunahitaji kuwafikia na kuwapa misaada ya kisheria” alisema.

Mtemo Rehema maluma ni miongoni mwa wateja waliwahi kupata huduma katika shirika la msaada wa kisheria Mingoyo alisema kuwa uwepo wa mashirika hayo ya usaidizi wa kisheria umekuwa msaada mkubwa hasa kwa wananchi wenye uwezo wa chini kwa kuwa mashirika huduma zake hutolewa Bure bila malipo 


“Wananchi wengi tunaweza kufikisha malalamiko yetu hapo tofauti na maeneo mengine ambapo inaweza kukulazimu kulipia kiasi Fulani cha fedha ili uipate haki yako mathalani ukianza kumtafuta wakili moja kwa moja lazima utalipia fedha lakini endapo utayatumia mashirika haya uwezi kulipia fedha yoyote ” alisema Maluma.

No comments:

Post a Comment