Monday, February 24, 2020

WANACHAMA WA CHADEMA MTAMA WAJIUNGA CCM

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

Ngome ya Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) kata ya Majengo Halmashauri Mtama yateketezwa kwa kuzinduliwa shina la Wakereketwa wa chama cha Mapinduzi CCM Kambalage katika Kata hiyo.

Uzinduzi huo umefanyika februaari 22 na katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM Taifa Dkt, Bashiru Ally ulioambatana na kupokea kadi ya muasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kata ya Majengo Halmashauri ya Mtama Namkuva Lihengelebwede pamoja na ugawaji wa kadi za mabalozi wa chama hicho zaidi ya 1800.

Inaelezwa kuwa awali mwaka 2015 kata ya majengo na Mtama katika halmashauri hiyo ni miongoni mwa ngome kongwe za chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) iliyokuwa ikitumika na chama hicho kupanga mikakati mbali mbali wakati wa uchaguzi mkuu.

Akizungumza mara baada ya kuzindua Shina hilo Katibu mkuu wa chama cha Mapinduzi CCM Taifa Dkt, Bashiru amewataka wanachama wa chama hicho kutumia mashina ya wakereketwa kuwa vijiwe vya kazi ya kuwashawishi wapinzani kujiunga na chama cha Mapinduzi (CCM).

“hawa watu huwa hawaji peke yao wanakuja na watu nyuma yao, wanakuja na kadi zao na wanakuja na siri zao, wanakuja na mikakati yao pia, kwa hivyo tumieni vijiwe hivi kuwaita na leo nimefurahi kumpata muasisi wa Chadema hapa nakupongeza sana” alisema Dkt, Bashiru. “

Chama cha Mapinduzi CCM ni Chama cha Kitaifa na ni chama cha wananchi wote hivyo tunavyompata mwananchama mmoja mpya ndio tunaongeza nguvu katika chama chetu hivyo ni wajibu wetu kama wana CCM kuwapa heshima watu hawa wanaokuja kwetu” alieleza Dkt Bashiru.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mtama Nape Nnauye alisema kuwa kitendo cha Rais Magufuli kuchagua Eneo la Mtama kuwa Halmashauri kimekuwa mwarobaini wa kufuta upinzani katika kata za mtama na majengo katika Halmashauri hiyo.

Alisema tangu kata hiyo ya Mtama kuwa Makao Makuu ya Halmashauri pamoja na mambo mengine yanayofanywa ya utekelezwaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM wananchi wa maeneo hayo wameendelea kuwa na imani na Rais wao.

Kwa upande wake Namkuva Lihengelebwede Muasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kata ya Majengo na Mtama Halmashauri ya Mtama alisema kuwa miongoni mwa vitu vilivyomshawishi kujiunga na Chama Cha Mapinduzi CCM ni baada ya Rais Magufuli kuifanya Mtama kuwa Makao Makuu ya Halmashauri.

“Kitendo cha Mheshimiwa Rais kuifanya mtama kuwa Halmashauri mimi na wenzangu tukaona ni vyema tukajiunga na Chama Cha Mapinduzi CCM ili kumuunga Mkono Rais wetu kwa ajili ya Maendeleo ya Mji wetu” alieleza Lihengelebwede.

No comments:

Post a Comment