Friday, February 21, 2020

WANAFUNZI KILWA HUTEMBEA UMBALI MREFU KUFUATA SHULE.

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

ZAIDI ya wanafunzi 260 wanaosoma katika Shule ya msingi Hotel tatu katika kata ya Hoteli tatu Wilayani Kilwa Mkoani Lindi hulazimika kutembea umbali mrefu kwa zaidi ya masaa matatu ili kufuata huduma hiyo ya shule jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao.

Hayo yameelezwa na mkuu wa Shule hiyo ya Hotel tatu Iddy Manonji hivi karibuni alipokuwa anazungumza na bagamoyo blog ofisini kwake

Kwa mujibu wa mkuu wa shule huyo wa shule wanafunzi hao ni kutoka kitongoji cha kalashi, kibaoni na Manyuli Mnonji alisema kutembea umbali mrefu kwa wanafunzi hao kunafanya hali ya kitaaluma kwao iwe inashuka kutokana na kufika shuleni wakiwa wamechelewa huku wakiwa wamechoka sana hali inayopelekea kutosoma vizuri

Alisema kutokana na umbali huo pia wazazi wa maeneo hayo wanashindwa kuwapeleka watoto wao wadogo kwa ajili ya kuanza madarasa ya awali kwa kuhofia usalama wao njiani ukizingatia hali ya mapoli na vichaka vilivyomo.

Kwa upande wake Hamida Saidi (11) mwanafunzi wa Darasa la tatu anaishi kitongoji cha mayuli alisema kuwa yeye na wenzake hulazimika kutembea alfajili licha ya kuwa na msitu na vichaka njiani ili waweze kuwahi vipindi darasani

“tukitoka saa 11 asubuhi nyumbani kwetu, tunafika shuleni saa mbili tukiwa tumechoka wakati mwingine tunasinzia darasani kwa sababu ya kukatisha katisha usingizi lakini hata tunaporudi tunafika nyumbani usiku sana kama ukiwa peke yako wakati mwingine unaogopa kutembea pekeyako” alisema Halima

Nae Fatuma mavumbi kutoka kitongoji cha kalashi alieleza changamoto nyingine wanayokabiliana nayo ni pale wanapofika shuleni wakiwa wamechelewa na kukuta mwalimu ameshaanza kufundisha hulazimika kuanzima dafutari za wanafunzi wenzao ili kuandika ambapo wakati mwingine unanakili na makosa ambayo aliyafanya mwanafunzi mwezio.

Mavumbi pia alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kujenga shule karibu na maeneo yao ili kuwapunguzia adha ya kutembea umbli mrefu kufuata huduma hiyo.

Nae mtendaji wa kijiji hicho abdalah shante alisema kuwa Kutokana na kutembea kwa muda mrefu pamoja na njia wanazotumia watoto hao wanajikuta hali ya ulinzi na usalama sio rafiki kwani jambo lolote linaweza kutokea kati kati bila ya mzazi au mwalimu kufahamu kwa haraka.

Kwa upande wake ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri hiyo Husen Kitingi amekili kuwepo kwa changamoto hiyo huku akieleza kuwa jitihada zinazochukuliwa kwa sasa ni kuanzisha shule shikizi katika vitongoji ambavyo vipo mbali na huduma hiyo ya shule

"Kama Halmashauri tunatarajia kuanzisha shule shikizi zaidi ya 20 katika vitongoji ambavyo vipo mbali na huduma ya shule ambapo tunashirikiana na wanajamii husika wa maeneo hayo"

No comments:

Post a Comment