Thursday, February 13, 2020

WAZIRI KALEMANI AWASHA UMEME KIJIJI CHA MPENDA HALMASHAURI YA MTAMA LINDI.

 Waziri wa nishati, Dkt. Medard Kalemani, akikata utepe kuashiria kuwasha umeme katika kijiji cha Mpenda Halmashauri ya Mtama mkoani Lindi.
....................................................
 
NA HADIJA HASSAN, LINDI.

Huwenda Ndoa za wakaazi wa kijiji cha Mpenda halmashauri ya Mtama Mkoani Lindi zikanusurika kuvunjika baada ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard kalemani kuwasha umeme katika kijiji hicho ambao pamoja na mambo mengine utasaidia kuzalisha maji.

Akitoa salamu za Mkoa pamoja na kuwasalimu Wananchi wa Mpenda Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Godfrey Zambi alisema kuwa kwa muda mrefu Wananchi wa Kijiji hicho walikuwa wakiikosa huduma hiyo ya Maji kutokana na kukosa nishati ya Umeme ya uhakika.

Ndemanga alisema baada ya kuwashwa kwa umeme huo sasa ni muda wa Mamlaka ya Maji safi na maji taka Mkoani humo Luwasa kuanza mikakati ya kufikisha maji katika kijiji hicho.

“hapa mpenda Mh, Waziri, baada ya leo kuwa umewasha umeme, tayari watu wa maji Luwasa wamesema na wao wanakuja kwa sababu wanauhakika sasa wa umeme, kwa hivyo umeme huu maana yake pamoja na matumizi mengine ya kibinaadamu lakini pia utavuta maji” alisema Ndemanga.

Akizungumzia changamoto hiyo ya maji diwani wa kata ya Mtama Hassan kunyong’onyea alisema kuwa changamoto hiyo imedumu kwa zaidi ya miaka 15 ambapo zaidi ya wakazi 1,280 wa kijiji hicho hutegemea kisima kimoja kupata huduma hiyo.

Hata hivyo Kunyong’onyea alisema Kisima kinapatikana umbali wa kilomita mbili kutoka kijijini hapo ambapo hata hivyo wananchi wanaokwenda kufuata maji wanalazimika kusubiri kwa zaidi ya masaa matatu mpaka manne ili kupata huduma hiyo.

Alisema hali hiyo ya kusubiri maji kwa muda mrefu inapelekea shughuli nyingi za kiuchumi za wananchi hao kudolola na mahali pengine hata kupelekea migogoro inayopelekea kuvunjika kwa Ndoa.

Kunyong’onyea aliongeza kuwa sasa yupo muwekezaji ambae amechimba kisima chake ambapo anauza maji kwa wananchi hao kwa shilingi 150 /= kwa ndoo yenye ujazo wa lita 10 na shilingi 250/= kwa dumu la lita 20 ambapo hata hivyo kulingana na kipato cha wananchi hao wengi wao wanashindwa kumudu ghalama hiyo.

Nae Amina Dadi Mkazi wa kijiji cha Mpenda Alisema Ndoa nyingi zinaingia kwenye migogoro kwa kile kinachodaiwa kuwa wanawake wanasingizia kigezo cha kufuata maji wakati wanaenda kufanya mambo yao kwa wanaume wa pembeni.

“licha ya kuwa wanaume zetu wanafahamu changamoto hii ya upatikanaji wa maji lakini bado tukirudi nyumbani kwa kuchelewa wakati mwingine tunapigwa au tunapewa taraka hivi juzi tuu kiangazi cha mwaka uliopita wapo wanawake waliopewa talaka na waume zao kwa kuchelewa kurudi nyumbani walipokwenda kufuata maji” Aliongeza Amina.

“kama kweli shida ilikuwa ni umeme sasa umeme umeshafika tunaiomba Serikali utufikirie sisi wanawake wa Mpenda tunateseka sana jamani, wakati mwingine tunakutana na chui simba huko tunakofuata maji” Alisema amina.
 
 Waziri wa nishati, Dkt. Medard Kalemani, akikabidhi kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) kwa wananchi wa kijiji cha Ng'au Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa.

 Waziri wa nishati, Dkt. Medard Kalemani, akisalimiana na wananchhi mbalimbali katika kijiji cha Ng'au Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa. 

No comments:

Post a Comment