Wednesday, February 26, 2020

MGALU ATAKA UMEME VIJIJINI UONGEZE UFAULU KWA WANAFUNZI.

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

NAIBU Waziri wa Nishati Subira Mgalu ametoa Rai kwa vijiji vyote ambavyo tayari vimeunganishwa na huduma ya Umeme, kupitia Mradi wa Umeme Vijijini (REA) kuitumia fursa hiyo kuboresha ufaulu pamoja na kuinua kiwango cha elimu katika Maeneo yao.

Mgalu aliyasema hayo alipofanya ziara ya siku moja katika Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi kwa lengo la kukagua maendeleo ya Mradi huo wa Umeme vijijini (REA) pamoja na kuwasha umeme katika vijiji vya Naluleo, Makata na Mengele Wilayani humo.

Akizungumza na wananchi, Walimu pamoja na Wanafunzi baada ya kuwasha umeme katika Shule ya Msingi Naluleo, Mgalu alisema ni mategemeo ya Serikali kuwa baada ya umeme kufika katika maeneo yao utaboresha na kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi kutokana na mazingira wezeshi ya kusoma na kujifunzia muda wote.

Aidha, Mgalu pia aliwaasa wanafunzi wa kike hapa Nchini kuepuka vishawishi kwa vijana wakiume pamoja na kuwataka walimu pamoja na Wazazi kuwa walinzi namba moja wa wanafunzi hao wakike kuhakikisha hawakatishi masomo yao kwa kupata ujauzito.

“Niwaombe sana hii sio kazi ya mzazi au mwalimu peke yake, nikazi yetu sote tunapomuona mtoto wa kike anafanya vitendo hivyo tumkemee, sisi walimu tuwe chachu hasa walimu wa kiume inatia uchungu kuona mwanafunzi wa kike anapata ujauzito kisha mwalimu ndio anahusishwa iwe ni ya kweli au kwa kusingiziwa hiyo sio sawa” alisema Mgalu.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Liwale Sara chiwamba alisema kuwa Swala la kutokomeza mimba kwa wanafunzi ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele katika Mkoa huo wa Lindi hasa kupitia kampeni ya “tumsaidie akue asome mimba baadae” yenye lengo la kumfanya mtoto wa kike atimize ndoto zake.

Kwa upande wake Abdull Mohamdi mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya Msingi Naluleo alisema kuwa upatikanaji wa umeme huo utakuwa mkombozi kwa walimu na wanafunzi hasa wakati wa kujiandaa na mitihani kuweza kujisomea nyakati za usiku.

“Baada ya umeme huu sasa wanafunzi tutakuwa na muda wa kutosha wa kuweza kujisomea kwa sababu hatutakuwa na shida tena ya kutafuta nishati ya umeme kama zamani “ alieleza.

No comments:

Post a Comment