NA VICTOR MASANGU, BAGAMOYO
MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo Zainabu Kawawa
ambaye pi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama (KUU) amepiga marufuku ngoma
na miziki ambayo inafanyika nyakati za usiku bila utaratibu maarufu
kama ‘Vigodoro’ kwani zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa mmomonyoko wa
maadili kwa wananchi.
Agizo hilo amelitoa wakati
akizungumza na wananchi wa Kata ya Nianjema, wadau wa maendeleo pamoja na wakuu
mbali mbali wa idara wakati wa mkutano wake wa kikazi kwa ajili ya kusikiliza
kero na changamoto mbali mbali za wananchi kwa lengo la kuweza kuzitafutia
ufumbuzi pamoja na kuweka mipango madhubuti kwa ajili ya kuleta chachu ya
maendeleo.
Zainabu alisema kwamba katika
baadhi ya maeneo ya Wilaya yake kumekuwepo wimbi la ngoma ambazo
zinachezwa nyakati za usiku na kupelekea kero na usumbufu mkubwa kwa watu
wengine hivyo ameamua kuchukua hatua ya kupiga marufuku hali hiyo kwa
lengo la kuondokana na mambo mbali mbali ambayo yamekuwa yakijitokeza hasa
katika wakati wa usiku.
“Kuanzia leo katika mkutano huu napenda
kusema napiga marufuku kabisa mambo ya vigodoro vya usiku kwani vimekuwa ni
kero sana na vinachangia kwa kiasi kikubwa katika kuvunja maadili ya Mtanzania
na kwamba katika hili nitahakikisha ninalisimamia kwa ukaribu mno ili kukomesha
kabisa kuwepo kwa hali hii katika Wilaya ya Bagamoyo,”alifafanua Zainabu.
Aidha Mkuu huyo alibainisha kwamba
wananchi wa Bagamoyo kwa sasa wanatakiwa kubadilika na kuwa na mtazamo chanya
kwa kushiriki kikamilifu katika shughuli mbali mbali za miradi ya maendeleo
kuliko kutumia muda wao mwingi katika kukesha nyakati za usiku wakicheza ngoma
ambazo hazina faida yoyote katika Taifa la Tanzania.
“Mimi kikubwa ninachotaka kuwaambia
hasa wananchi wa Wilaya ya Bgamoyo tuachane kabisa na kujikita zaidi katika
kukesha kwenye vigodoro, ni vyema zaidi mkatumia fursa mbali mali
zilizopo mkajishughulisha katika shughuli za kujipatia kipato ili kuweza
kuondokana na wimbi la umasikini hivyo ni rai yangu wote tukashirikiana
katika kuleta maendeleo na sio kukesha kwenye vigodoro ambavyo ni havina faida
yoyote ile,”alisema Zainabu.
Pia Mkuu huyo wa Wilaya alifafanua
kwamba mtu yoyote ambaye anahitaji kufanya shughuli yake ya usiku ni lazima
apatiwe kibali maalumu kutoka katika Ofisi yake kwa kuzingatia sheria na
utaratibu ambao utakuwa umewekwa,ili kuhakikisha mambo yote ambayo yanakuwa
yanajitokeza nyakati za usiku ikiwemo masuala ya uhalifu na wizi
yanakomeshwa kwa kiasi kikubwa.
Katika hatua nyingine ametoa onyo
kali kwa wale wote ambao watabainika kukiuka agizo lake ambalo amelitoa na
kwamba atahakikisha anawachukulia hatua kali za kisheria wale wote ambao
watabainika bado wanaendeleo kinyemela kujihusisha na masuala ya kupiga
ngoma za usiku na vigodoro bila ya kuwa na kibali maalumu.
Nao baaadhi ya wananchi ambao hawakuta
kutaja majina yao walimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo kwa hatua ambayo
ameifanya ya kupiga marufuku kabisa mambo ya vigodoro hasa katika nyakati za
usiku kwani yamekuwa ni tatizo kubwa kutokana na kuwepo kwa matukio mbali mbali
ambayo yanasabisha momonyoko wa maadili hasa kwa vijana.
“Kwa kweli sisi kama wananchi wa Wilaya
ya Bgamoyo hili agizo la Mkuu wetu kupiga marufuku ngoma za usiku maarufu
vigodoro sisi tunamuunga mkono kwa asilimia mia moja kwani imekuwa ni kero sugu
ya siku nyingi na wakati mwingine yani watu hatulali kabisa na kingine kuna
baadhi ya matukio ambayo yanafanyika hivyo kwa hatua hii itaweza kusaidia
kuondoa na kupunguza kabisa changamoto amabzo zimekuwa zikijitokeza katika
maeneo ambayo tunaishi,”walisema.
Kwa upande wake mmoja wa wadau wa
maendeleo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nianjema Abdul Pyalla, alisema kwamba
suala hilo la vigodoro ni kweli limekuwa ni kero kubwa kwa wananchi hivyo
atahakikisha anashirikiana bega kwa bega na Mkuu wa Wilaya pamoja na
wananchi husika katika mitaa mbali mabli kwa lengo la kuwaelimisha zaidi kuhusu
umuhimu wa kutumia muda wao katika shughuli za maendeleo kuliko kukesha kwenye
ngoma.
Baadhi ya Wananchi wa Wilayani Bagamoyo
wakiwa wametulia kwa makini kumsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo ambaye
aliitisha Mkutano maalumu kwa ajili ya kuzungumzia mambo mbali mbali ya
maendeleo kwa wakazi wa kata ya Njia njema pamoja na kuwasikiliza changamoto
zao. (PICHA NA VICTOR MASANGU)
No comments:
Post a Comment