Tuesday, February 11, 2020

WAANDIKISHAJI DAFTARI LA KUDUMU LA MPIGA KURA WAAPISHWA RASMI CHALINZE


Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la Chalinze Bi Amina Kiwanuka, amewaapisha rasmi, waandikishaji wasaidizi 319 na na watumiaji wa mashine za kuandikishia wapiga kura yaani "BVR" 319. Waandikishaji hao waliapishwa katika Ukumbi wa shule ya sekondari ya Lugoba baada ya kupata mafunzo ya namna ya uandikishaji wa wapiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura.


Kiwanuka katika hotuba yake ya uzinduzi wa mafunzo ya uandikishaji aliwataka wote walioteuliwa kufanya zoezi hili muhimu la kitaifa kwa umakini,uadilifu na weledi wa hali ya Juu,kwani wameaniwa hivyo wazingatie sheria, taratibu na kanuni zinazotumika katika zoezi hili.


Aidha Afisa Mwandikishaji wa Jimbo amewataka kuzingatia muda wa kufungua vituo na kufunga."Mnatakiwa kuutumia vizuri muda wa uandikishaji kwani zoezi hili litafanyika kwa muda wa siku Saba tu kuanzia tarehe 14/02/2020 hadi tarehe 20/02/2020." Kiwanuka alisisitiza.


Bi Kiwanuka katika hotuba yake alitoa wito kwa wananchi wote katika halmashauri ya Chalinze na Jimbo la Chalinze kujitokeza kwa wingi ili kuja kujiandikisha lakini pia kurekebisha taarifa zao endapo Pana uhitaji wa kufanya hivyo,amewaagiza watendaji wa kata,watendaji wa vijiji,wenyeviti wa vijiji,wenyeviti wa vitongoji na vyombo vya Habari kuwahamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi kuja kujiandikisha.


Hata hivyo aliwataka wananchi kutoa taarifa sahihi kuhusu ndugu na jamaa waliofariki au kufungwa ili waweze kuondolewa katika daftari la wapiga kura na hatimaye kuwa na watu sahihi katika daftari hilo.


IMETAYARISHWA NA KITENGO CHA HABARI,MAWASILIANO NA UHUSIANO
HALMASHAURI YA WILAYA YA CHALINZE


No comments:

Post a Comment