Tuesday, February 4, 2020

KITONGOJI CHA UKUNI BAGAMOYO WATENGA VIWANJA VYA MICHEZO

Na Omary Mngindo, Bagamoyo.

Kitongoji cha Ukuni, Kata ya Dunda wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani wetenga eneo lenye ekari zaidi ya tatu kwa ajili ya viwanja vya michezo.

Hayo yamebainishwa na diwani wa Kata hiyo Dickson Makamba, mbele ya Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Dawson Shigera katika mkutano Mkuu uliogubikwa na changamoto lukuki ikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara maeneo yaliyotelekezwa.

Kauli ya diwani Makamba ilitanguliwa na malalamiko ya udogo wa uwanja unaotumika na vijana kitongojini hapo, hali inayotokana na eneo hilo kuwa na ardhi ya kutosha lakini walioyanunua wameyaacha hivyo kuwa mapori.

"Naomba nizungimzie malalamiko ya Dkt. Omary kuhusiana na ufinyu wa eneo la vijana kushiriki michezo, Kitongoji chetu kina eneo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari tatu zilizotengwa kwa ajili ya viwanja vya michezo, ambapo pia tunaweza kuweka mabembea ikawa sehemu ya vyanzo vya mapato," alisema Makamba.

Awali Dkt. Omary alielezea masikitiko yake kuhusiana na changamoto hiyo ya ukosefu wa uwanja wa michezo, huku akiuelezea uwanja uliopo eneo hilo ambalo ndio linalofanyikia mikutano kuwa finyu, ukilinganisha na mipangilio mizuri iliyopo.

"Kitongoji cha Ukuni kina eneo kubwa na mji wake kuwa katika mipango iliyobora, lakini cha kusikitisha ni kukosekana kwa viwanja vya michezo kwa vijana wetu, huku sehemu kubwa ya mji ukiwa umezungukwa na mapori yanayomilikiwa na watu waliopo nje ya Ukuni," alisema Dkt. Omary.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Shigera alianza kuwapongeza watangulizi wake kwa namna walivyokisimamia katika nyanja mbalimbali, huku akiwaomba wana-Ukuni kuwapatia ushirikiano ili kwa pamoja wakipatie maendeleo Kitongoji chao.

"Maendeleo tunayoyataka hayawezi kufikiwa kama sisi wananchi tutakuwa wagumu kufika kwenye mikutano, tumezungumzia viwanja vya michezo sekta inayoongoza kuwapatia ajira wa-Tanzania waliowengi," alimalizia Mwenyekiti huyo.

No comments:

Post a Comment