Tuesday, February 4, 2020

KAWAMBWA ASHUHUDIA MRADI WA MAJI CHOMBE JUU

Na Omary Mngindo, Bagamoyo.

WAKAZI wa Vijiji na Vitongoji vilivyomo ndani ya Kata zinazounda Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wanatarajia kunufaika na usambazaji wa maji kutoka kwenye vyanzo vilivyopo kweye maeneo yao.

Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo hilo Dkt. Shukuru Kawambwa, akizungumza na wakazi wa Kitongoji cha Chombe Juu Kata ya Yombo, aliposhuhudia matofali na mabomba yatakayojenga kituo cha kuchotea maji sanjali na mabomba ya kusambazia kwenye vituo vitatu.

Mbele ya James Kionaumela Mhandisi wa Maji (RUWASA), Makamu Mwenyekiti wa halmashauri Mohamed Usinga ambaye ndie diwani wa Kata hiyo na Hassani Wembe diwani wa kata ya Kiromo, Dkt. Kawambwa alisema kuwa juhudi hizo za serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, zimedhamiria kuwakomboa wananchi.

"Niliwahi kuwaleta marafiki zangu hapa kuchimba visima viwili kwa thamani ya zaidi ya shilingi milioni 9, lakini kwa bahati mbaya maeneo hayo moja halikuwa na maji kabisa, lingine maji yake hayakuwa katika ubora, yalikuwa na rangi sana," alisema Dkt. Kawambwa.

Kwa upande wake Mhandisi Kionaumela aliishukuru serikali kwa kuanzisha chombo kinachoitwa RUWASA, kinacholenga kushugbulikia usambazaji wa maji kutoka kwenye vyanzo na kuwasambazia wananchi, lengo ni kumtua ndoo mwanamke.

"RUWASA tumepewa jukumu la kuwasambazia maji wananchi, kutoka katika visima tusambaza mabomba ili maji hayo yawafikie wananchi, hapa Chombe Juu leo tumeleta matofali na mabomba kwa ajili ya kazi hiyo," alisema Kionaumela.

Makamu Mwenyekiti Usinga alisema kuwa juhudi hizo zinalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji, huku akimshukuru Mbunge Dkt. Kawambwa kwa juhudi zake za kuwatafuta marafiki kwa ajili kuchimba visima vya maji.

"Tulikuja kutoa ahadi ya maji katika eneo hili, leo tumefika hapa chini ya Mkuu wetu wa msafara Dkt. Shukuru Kawambwa anayefanyakazi kubwa ya kuwatafuta marafiki kwa ajili ya kuendeleza mradi wa maji uliopo kwnye eneo hill," alisema Usinga.

Nae Wembe hakusita kuanza kumpongeza Dkt. Kawambwa kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha wananchi wake wanaondokana na changamoto ya maji katika maeneo yao.

No comments:

Post a Comment