Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Profesa William
Anangisye, ofisini kwa Waziri Mkuu Mjini Dodoma, Machi 16, 2018.
...........................................
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema ni umuhimu mfumo wa ufundishwaji wa wanafunzi wa
vyuo vikuu nchini ukaboreshwa ili wanapomaliza waweze kujiajiri.
“Kumekuwa
na tatizo kubwa la wasomi wetu kuwa na mtazamo kwamba wanapomaliza masomo yao lazima waajiriwe. Upo
umuhimu wa kubadili mtazamo huo kwa kuwapa mbinu zitakazowawezesha kujiajiri.”
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Machi 16, 2018) alipokutana na kufanya
mazungumzo na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. William
Anangisye, ofisini kwake mjini Dodoma.
Amesema
wanafunzi hao wanapomaliza wanatarajiwa wawe na uwezo wa kubuni mbinu
mbalimbali za kujiajiri na kuondokana na mtazao wa kusubiri ajira za kuajiriwa
maofisini.
Waziri
Mkuu amesema wasomi hao wanaweza kuchukua kauli mbiu ya Rais Dkt. John Magufuli
ya uchumi wa viwanda kwa kuanzisha kilimo cha mazao mbalimbali yatakayotoa
malighafi za viwandani.
Pia
Waziri Mkuu amesema wasomi hao wanaweza kujikita katika shughuli za uchimbaji
wa madini au usindikaji wa mazao mbalimbali, hivyo tayari watakuwa wamejiajiri
kwa sababu ajira si za ofisini pekee.
Aidha,
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyestaafu
Profesa Rwekaza Mukandara kwa kazi nzuri aliyoifanya kipindi cha uongozi wake.
Kwa
upande wake, Profesa Anangisye amesema mzigo aliopewa wa kuiongoza taasisi hiyo
si mwepesi, hivyo ameahidi kufanya kazi kwa bidii na hatokwenda kinyume na
matarajio ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Kiongozi
huyo amesema katika kuhakikisha wanaboresha masomo chuo hapo wameanzisha skuli
ya kilimo na uvuvi, hivyo wanatarajia kuanzisha mashamba ya mfano kwa ajili ya
mazao mbalimbali.
No comments:
Post a Comment