Tuesday, March 13, 2018

MKOA WA PWANI WAJIPANGA KUDHIBITI MAGHALA YA KOROSHO YA VICHOCHORONI



Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo (wa pili kushoto) alipotembelea ghala linalomilikiwa na kampuni ya RK Chudasama Ltd wilayani Mkuranga,(wa kwanza kushoto)mkurugenzi kampuni hiyo ,Sundeep Chudasama ,wa kwanza kulia Katibu wa CCM Mkuranga, Shilla na wa pili kulia mkuu wa wilaya hiyo,Filberto Sanga
...............................................

SERIKALI mkoani Pwani, inatarajia kuchukua mbinu mbadala ya kukodi ghala lenye ubora na kuendelea na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia korosho ili kupambana na vyama ushirika vya msingi (AMCOS) vilivyokuwa vikitumia maghala ya vichochoroni na majumbani yasiyo na viwango.

Aidha ,imesema haitokubali kutumia maghala ya vyama hivyo katika msimu ujao na kudai mkoa umechoka kudang’anywa na kuchafuliwa sifa ya nchi kwenye soko la nje.

Mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo, aliyasema hayo wakati alipotembelea ghala la kisasa linalomilikiwa na kampuni ya RK CHUDASAMA Ltd, wilayani Mkuranga.

Alieleza,serikali imeshamlipa malipo ya awali sh.bilioni moja mkandarasi wa ujenzi wa ghala la kuhifadhia korosho wilayani Mkuranga, inalojengwa na kampuni ya BQ Contractors Ltd .

Ndikilo alisema endapo ghala hilo litakamilika mwezi sept ,litatumika lakini kama litachelewa ,watakodisha ghala la uhakika kwa ajili ya wakulima wa Mkuranga ambapo wanatarajia kuwa na tani 15,000 hadi 20,000 za korosho kwa msimu unaokuja.

Anasema’,”Ghala hilo linajengwa na bodi ya korosho Tanzania.lengo kubwa ni kuwa na maghala makubwa yatakayohifadhi korosho Kibiti, Mkururanga na Kibaha.

Kwa mujibu wa Ndikilo,lengo ni kupambana na udanganyifu wa zao korosho maana kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani mkoa huo haukuwa ukitumia maghala rasmi .

“Ghala hili mnalojenga RK CHUDASAMA lipo kwenye kiwango ,limekamilika kwa asilimia 90 tunaomba muache milango wazi,kama tutakuja kukodisha kuhifadhi korosho zetu mtupokee”alisisitiza Ndikilo.

Hata hivyo ,alisema serikali imeona ianze kuchukua hatua mapema ili kuepukana na udang’anyifu na hujuma zilizojitokeza msimu huu unaomalizika .

Ndikilo alielezea, kuna baadhi ya AMCOS zilihusika kuchakachua na kutelemsha ubora wa korosho pamoja na kuweka mawe na michanga kwenye magunia ya korosho zilizokuwa zinauzwa kwenye minada .

“Hali hii imetia doa ,,Kuna watu wachache wanataka kuwaharibia wakulima ambao ni asilimia 80 ambayo wanajishughulisha na kilimo,lakini nawapa taarifa serikali haitakubali hata kidogo kuona ubabaishaji huu ukiendelea”alisema Ndikilo.

Mkurugenzi wa RK CHUDASAMA Ltd ,Sundeep Chudasama alikubali kushirikiana na serikali kwa kutoa ghala lake kulingana na makubaliano watakayowekeana.

Alieleza yupo tayari kupangisha ghala hilo ambalo ujenzi wake unakaribia kukamilika na kampuni yake inaendelea kujenga maghala ikiwemo jijini Dar es salaam ambako anayapangisha.

Sundeep alifafanua,mipango yake ni kuendelea kujenga viwanda na ameshajenga maghala mawili wilayani Mkuranga na anawasiliana na wawekezaji wengine ili waje kuwekeza nchini.

“Mie ni mtanzania halisi,nimesoma hapa ,sina tatizo tutashirikiana pamoja na nina ahidi kutoa ghala hili ,kwa mipango na utaratibu tutakaojiwekea,ili kila upande unufaike”alisema Sundeep.

Nae katibu tawala msaidizi uchumi na uzalishaji,mkoani Pwani ,Shangwe Twamala alisema kwasasa mkoa umejiwekea mkakati wa kujenga maghala makubwa matatu ambayo yataondoa changamoto zilizojitokeza hivi karibuni.

Alisema ,wajibu wa serikali ni kuwaunga mkono wakulima ,kwa kuhakikisha wanapata manufaa na tija kupitia jasho wanalolitoa kwa kujishughulisha na kilimo chao.

Twamala ,aliwaasa wale wote wanaojiingiza katika udalali badala ya kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani na kuvitaka vyama vya msingi vya ushirika kuacha kujiingiza kwenye wizi na kuwakandamiza wakulima.

Mwishoni mwa mwezi desemba mwaka 2017,viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) kumi ,walikamatwa na kuhojiwa kutokana na kosa la kufanya udanganyifu wa ubora na uzito wa korosho ,na uchunguzi unaendelea .

No comments:

Post a Comment