Tuesday, March 20, 2018

MSITU WA ZIGUA SASA UMEREJEA KATIKA HALI YAKE YA KAWAIDA.


Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mh. Alhaj, Majid Hemedi Mwanga akionyesha sehemu ya makazi ya watu waliokuwa wamevamia msitu wa Zigua hivi karibuni katika Doria maalu ya kukagua msitu huo iliyowashirikisha watendaji kutoka TFS wilaya ya Bagamoyo na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ambapo kwa pamoja wamejiridhisha kwamba hakuna mvamizi aliykuwemo ndani ya msitu huo kwa sasa.
........................................

Hifadhi ya msitu wa zigua imerejea katika hali yake ya kawaida baada ya kuwaondoa wavamizi ndani ya msitu huo.

Akizungumza na bagamoyokwanza blog amara bada ya kufanya doria maalum katika msitu huo, Kaimu Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) Halmashauri ya Chalinze David George Ntemi, alisema hali ya msitu huo kwa sasa inaridhisha kutokana na miti kushamiri na baadhi ya wanyama kuonekana kurejea ndani ya msitu huo ambao awali walianza kutoweka.

Alisema  hifadhi hiyo ya msitu wa Zigua, ulikuwa umeharibiwa na wananchi ambao walivamia kwa kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo kulima, kukata miti na kuchungia mifugo hali iliyopelekea msitu kuharibika asili yake na wanyama kukimbia.

Aliongeza kwa kusema kuwa, mara baada ya kuwatoa wavamizi katika zoezi lililoshirikisha wilaya tatu za Bagamoyo, Handeni na Kilindi kwa sasa Hifadhi ya msitu wa Zigua kwa upande wa Bagamoyo uko vizuri baada ya kujihakikishia kuwa hakuna mtu hata mmoja ndani ya msitu huo kwa sasa.

Alisema Doria hiyo maalum imefanywa katika kipindi hiki ambacho tayari wakulima huandaa mashamba kwaajili kilimo cha mwaka hivyo lengo lilikuwa ni kujiridhisha endapo wakulima hao wamerudi au wameondoka moja kwa moja.

Aidha, alisema baada ya kuzunguuka eneo lote wapo watu wawili ambao waliozidisha mipaka yao na kuingilia sehemu ya msitu na kwamba tayari wameshapewa taarifa ya kuacha kupanda sehemu ya msitu ili kuepuka kuharibiwa mazao yao.

Akizungumzia umuhimu wa msitu huo Ntemi alisema msitu huo ni mapitio ya wanyama kutoka hifadhi ya taifa ya Saadani na kuelekea Mikumi.

Ntemi aliongeza kuwa, msitu huo pia ni chanzo cha maji cha mito ya saja na kigulu inayopeleka maji katika mto wami ambao unahudumia miji ya Chalinze na Bgamoyo.

Alisema msitu huo pia ni sehemu ya kuzalia wanyama ambapo kuharibika kwa msitu huo kutapelekea wanya hao kutoweka na hivyo kupoteza rasilimali za taifa.

Ntemi alisema kutunzwa kwa msitu huo kunapelekea kupatikana kwa mvua kwa wakati ambapo ukiharibiwa ni sababbu ya kutoweka kwa mvua hali itakayosababisha ukame katika ukanda huo.

Nae aliyekuwa akiongoza vikosi katika kuwatoa wavamizi Mkuu wa polisi wilaya ya Kipolisi Chalinze Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Janeth Magomi aliwataka wananchi wanaozunguuka msitu huo kutii sheria bila ya shuruti ili kuepuka usumbufu ambao wanaweza kuupata pindi wanapokaidi sheria.

Alisema viongozi wa Mkoa na wilaya kupitia mikutano mbalimbali na wananchi walishatoa maelekezo namna ya kuulinda msitu huo hivyo kila mwananchi akazingatia maelekezo ya viongozi na kuacha kuvunja sheria kwa makusudi.

Alisema kwa sasa hali ya msitu huo tulivu kwakuwa tayari wananchi wanaonekana kutii sheria bila ya shuruti.

Wananchi wa kata ya Kibindu waliozungumza na bagamoyokwanza blog walisema faida walizopata katika kuhamishwa kutoka kwenye msitu ni pamoa na kupata huduma za Afya, Barabara na Elimu.

Walisema katika maeneo ya msitu ilikuwa vigumu watoto kwenda shule na matibabu pale mtu anapoumwa lakini kwa sasa wanapata huduma zote kwa urahisi kwakuwa wapo katika makazi ya watu.
 Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mh. Alhaj, Majid Hemedi Mwanga akiwa na watendaji kutoka TFS wilaya ya Bagamoyo wakitabasamu baada ya kuona hali ya msitu wa mzigua imeanza kuridhisha.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Bagamoyo, ambae ni Mkuu wa Wilaya ya hiyo Mh. Alhaj, Majid Hemedi Mwanga (aliyeshika fimbo) akiongoza Doria maalum ya kukagua msitu wa Zigua.

 Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mh. Alhaj, Majid Hemedi Mwanga (kushoto) akifurahia jambo na wanakijiji waliotolewa ndani ya msitu wa Zigua kata ya Kibindu hivi karibuni wakati wa Doria maalum ya kukagua Msitu huo.

No comments:

Post a Comment