Monday, March 5, 2018

JK. ACHANGIA UJENZI WA SHULE KIBINDU WILAYANI BAGAMOYO.


 Rais Mstaafu wa awamu ya nne nchini Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete akiwasili shule ya msingi Kibindu, kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Mwanga, kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete.

Rais Mstaafu wa awamu ya nne nchini Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete, akizungumza katika shule ya msingi Kibindu iliyopo kata ya Kibindu Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo, wa kwanza kulia ni Mkewe Mama Salma Kikwete, wapili kulia ni Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Alhaj, Majid Mwanga na kushoto ni Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete.
......................................................
Rais Mstaafu wa awamu ya nne nchini Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete amechangia mifuko 450 ya Saruji ambapo kati ya hiyo mkewe mama Salma Kikwete amechangia mifuko 150 katika uenzi wa shule za Msingi Kibindu, Kweikonje, na Pera katika Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo.

Rais huyo mstaafu wa Tanzania ametoa mchango huo baada ya kutembelea shule hizo ambazo zinaendelea na ujenzi wa kuongeza vyumba vya madarasa ili kukabiliana na msongamano wa wanafunzi ambao wamekuwa wakiandikishwa kwa wingi kila mwaka.

Akitoa mchango huo Rais huyo Mstaafu amewapongeza viongozi wa wilaya, Mbunge pamoja na wananchi kwa kujitolea katika kuhakikisha shule hizo zinaongeza vyumba vya madarasa.

Alisema shule hizo zinamahitaji ya vyumba vya madarasa hivyo ushirikiano ndio njia pekee itakayoweza kusaidia ujenzi wa madarasa hayo.

Hata hivyo ametoa ushauri kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze kuona uwezekano wa kuigawa shule ya Msingi Kibindu ili kuondoa msongamano wa wananfunzi uliopo kwa sasa.

Aidha, alitumia fursa hiyo kumshukuru Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa (TANAPA) Allan Kijazi, kwa kutoa milioni 160 kwaajili kuchangia ujenzi wa shule mbili ikiwemo shule ya msingi Kibindu na Kweikonje.

Dkt. Jakaya alimuomba Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa (TANAPA) Allan Kijazi, kuangalia uwezekano wa kuongeza msaada katika shule ya Msingi Kibindu ili kuwaondolea adha ya msongamano wananfunzi wa shule hiyo.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema anaipongeza Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Shule ya msingi kibindu imeanzishwa mwaka 1952 ambayo kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 1407 ambapo mahitaji ya vyumba vya madarasa ni 32 na madarasa yaliyopo kwa sasa ni saba tu.
 Rais Mstaafu wa awamu ya nne nchini Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete akipokelewa na Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Hemed Mwanga mara baada ya kuwasili shule ya msingi Kibindu ambapo alienda kujionea ujenzi wa upanuzi wa shule hiyo.

 Rais Mstaafu wa awamu ya nne nchini Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete
akijenga ukuta wa madarasa yanayoendelea kujengwa katika shule ya msingi Kibindu, huku Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete akiwa saidia fundi kwa kumpa udongo Rais Mstaafu ili kazi ya ujenzi iendelee.
 Mke wa Rais Mstaafu wa Tanzania, Mama Salma Kikwete, ambae pia ni Mbunge wa kuteuliwa akishiriki kujenga ukuta wa madarasa yanayoendelea kujengwa katika shule ya msingi Kibindu.
 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Hemed Mwanga, (kulia) na Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete (kushoto) wakibeba mawe kwaajili ya kujaza kwenye vyumba vya madarasa vinavyotakiwa kumwagwa zege la jamvi katika shule ya Kibindu.
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Hemed Mwanga, akijenga ukuta wa madarasa yanayoendelea kujengwa katika shule ya msingi Kibindu.

Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete, akijenga ukuta wa madarasa yanayoendelea kujengwa katika shule ya msingi Kibindu, wakati walipotembelea shuleni hapo pamoja na Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete.

No comments:

Post a Comment