Sunday, March 18, 2018

MBEGU YA MAHINDI YA W. 21 09 YAZINDULIWA BAGAMOYO.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga ( wa pili kushoto mwenye miwani) akizindua rasmi Mbegu ya mahindi ya W. 21 09 katika msimu wa kilimo 2018. pamoja nae kulia ni Mkurugenzi wa fedha na utawala, Shabani Hussein kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na wapili kulia ni
mtafiti wa mbegu hiyo ya mahindi ya  W. 21 09 kutoka kituo cha utafiti Ilonga wilayani Kilosa, Mikidadi Hamidu.

Na Athumani Shomari
......................................

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga amezindua Mbegu bora ya Mahindi ya W. 21 09 katika msimu wa kilimo 2018 itakayotumika na wakulima wa mahindi kwaajili ya kuzalisha mahindi mengi na yenye ubora.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mkuu huyo wa wilaya alisema mbegu hiyo itawapa fursa wananchi wa Bagamoyo kuvuna mazao mengi na yenye ubora hali itakayowasaidia kukabiliana na soko la ajira wilayani humo.

Alisema wilaya ya Bagamoyo ipo katika ujenzi wa viwanda hivyo ili mwananchi aingie kwenye ushindani wa ajira anahitaji kuwa na chakula kitakachomuwezesha kuwa na utulivu wa akili na mwili.

Akizungumzia utafiti mkurugenzi wa fedha na utawala, Shabani Hussein kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) alisema tume hiyo inafadhili tafiti mbalimbali ikiwemo mbegu za mahindi na muhogo ili wakulima wapate matokeo mazuri ya kile wanachopanda.

Afisa mipango wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Bestina Daniel alisema mbegu hiyo ambayo imefanyiwa utafiti katika kituo cha Ilonga kilichopo Kilosa imetia michakato yote ya kuthibitishwa na kuidhinishwa kwaajili ya kuingia sokoni kwa matumizi.

Nae mtafiti wa mbegu hiyo ya mahindi ya  W. 21 09 kutoka kituo cha utafiti Ilonga wilayani Kilosa, Mikidadi Hamidu alisema Mbegu hiyo ya mahindi ina uwezo wa kutoa gunia 35 kwa ekari moja endapo mkulima atazingztia kanuni za kilimo cha mahindi.

Kwa upande wake, Afisa kilimo wa Mkoa wa Pwani George Kapilima alisema wilaya ya Bagamoyo inaongoza kwa kilimo cha mahindi Mkoani wa Pwani, huku zao la mahindi likishika nafasi ya pili baada ya zao la muhogo mkoani humo.

Alisema katika msimu wa kilimo wa mwaka 2016/2017 Mkoa wa Pwani ulizalisha tani laki moja na kumi 110,000 ambapo Halmashauri ya Chalinze iliyopo ndani ya wilaya ya Bagamoyo ilizalisha tani elfu sitini na tano 65,000 za mahindi.

Alisema mazao yanayoongoza mkoani Pwani ni Muhogo, Mahindi na Mpunga ambapo alisema mbegu hiyo ya W. 21 09 itasaidia kuongeza uzalishaji wa zao la mahindi wilaya ya Bagamoyo na Mkoa wa Pwani kwa ujumla.

 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga, akipanda mahindi ikiwa ni ishara ya kuzindua rasmi mbegu ya W. 21 09 katika kitongoji cha Kilemela kata ya Kerege wilayani Bagamoyo.

Afisa kilimo wa Mkoa wa Pwani George Kapilima kushoto
akipanda mahindi ikiwa ni ishara ya kuzindua rasmi mbegu ya W. 21 09 katika kitongoji cha Kilemela kata ya Kerege wilayani Bagamoyo.
 mkurugenzi wa fedha na utawala, Shabani Hussein kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) akizungumza katika uzinduzi wa mbegu mpya ya mahindi ya W. 21 09.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga ( wa pili kushoto mwenye miwani) akizindua rasmi Mbegu ya mahindi ya W. 21 09 katika msimu wa kilimo 2018. pamoja nae kulia ni Mkurugenzi wa fedha na utawala, Shabani Hussein kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na wapili kulia ni

mtafiti wa mbegu hiyo ya mahindi ya  W. 21 09 kutoka kituo cha utafiti Ilonga wilayani Kilosa, Mikidadi Hamidu, anaekabidhiwa ni Anna Macha kutoka kikundi cha Tupendane kijiji cha Kongo.

No comments:

Post a Comment