Tuesday, March 6, 2018

MARUFUKU MKAA KWENYE GARI ZA ABIRIA- DC BAGAMOYO.


Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga akiangalia Basi la abiria ambalo limebeba mkaa kwenye buti. 
 Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga akiangalia Basi la abiria ambalo limebeba mkaa kwenye buti. 
...............................................

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga amepiga marufuku ndani ya wilaya yake kupita mabasi ya Abiria ambayo yamebeba Mkaa.

Mkuu huyo wa wilaya ametoa kauli hiyo kwenye oparesheni maalum ya kukagua mazao ya misitu ambayo yanasafirishwa bila ya kuwa na kibali na kukwepa ushuru hali inayopelekea kuikosesha serikali mapato.

Alisema kila mwenye kusafirisha mazao ya misitu ikiwemo Kuni, Mbao, Mkaa na Miti ya ujenzi anapaswa kuwa na kibali kinachomruhusu kuvuna na kusafirisha huku akisisitiza kuwa ndani ya vibali hivyo yapo maelekezo ya wapi muhusika anapaswa kuvuna Mbao, Mkaa au Kuni.

alisema kwa kuzingatia sheria zilizowekwa ndio kutapelekea kulinda mapato ya serikali ambayo faida ya mapato hayo inarudi kwa wananchi kwa kuwatekelezea miradi mbalimbali ya maendeleo.

Katika Oparesheni hiyo maalum, mkuu wa wilaya ya Bagamoyo amebaini mabasi kadhaa Abiria yanayobeba mkaa hali inayohatarisha usalama wa abiria.

Alisema licha ya kukiuka sheria za usalama barabarani, ubebaji wa Mkaa katika mabasi ya Abiria ni hatari kwa usalama kwakuwa baadhi ya magunia ya mkaa yanakuwa na cheche za moto hali itakayopelekea gunia la mkaa kuwaka moto na hatimae Gari lote kuungua na kupoteza maisha ya watu wasio na hatia.

Aidha, aliwataka Abiria kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kubaini mabasi yote ya Abiria yanayobeba magunia ya mkaa ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheia zitakazokomesha tabia ovu katika sekta ya usafirishaji.

Kwa upande wao Abiria wa mabasi hayo walisema wanakerwa vitendo vya kupakia magunia ya mkaa kwenye mabasi ya abiria kwakuwa hutumia muda mrefu kupakia mkaa njiani.

Walisema katika safari kila mtu anamahitai na umuhimu wake wa kuwahi hivyo kitendo cha kucheleshwa kwasababu ya kupakia mkaa ni kutokujali umuhimu wa safari kwa abiria.

Nao makondakta wa mabasi yanayofanya safari katika barabara ya Chalinze Segera walisema wanalazimika kupakia mkaa ili kufidia kwakuwa kuna shida ya abiria ambapo Gari hutumbea bila ya kujaza na kupelekea kushindwa hata pesa ya kujaza mafuta.

Walisema gunia moja la mkaa wanasafirisha kwa bei ya shilingi elfu kumi ambayo ukizidisha kwa magunia kumi unaweza kupata pesa ya kuongezea kipato.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga, akiangalia magunia ya mkaa marefu yanayojulikana kwa jina la Shanga mbili, ambayo yapo kando ya barabara ya Chalinze Segera kwaajili ya kusubiri kupakiwa kwenye mabasi ya abiria, pamoja nae kulia ni Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFSA) Halmashauri ya Chalinze, David Ntemi, na wa pili kulia ni Kaimu meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFSA) kanda ya Mashariki, Suleiman Bulenga.
Basi hili limekutwa limepakia magunia kumi ya mkaa makubwa (shanga mbili) kutoka Kimange kuelekea Dar es Salaam, ambapo kila gunia moja hulipiwa shilingi Elfu kumi.

No comments:

Post a Comment