Kamanda wa polisi mkoani Pwani, kamishna msaidizi mwandamizi, (SACP) Onesmo
Lyanga, akizungumza na waandishi wa habari, ofisini kwake.
JESHI la polisi mkoani Pwani, linamshikilia Amiri Alalae (26)mkazi wa
Toptop, wilaya ya Bagamoyo kwa kosa la kusafirisha wahamiaji haramu 30 raia wa
nchini Ethiopia.
Kamanda wa polisi mkoani humo, Onesmo Lyanga, alisema tukio hilo limetokea
april 13 majira ya saa kumi usiku huko maeneo ya Kilomo kata ya Kilomo tarafa
ya Yombo.
Alieleza kuwa askari wa jeshi la polisi waliokuwa kwenye doria maeneo
mbalimbali ya wilaya ya Bagamoyo walifanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu hao
wakiwa wameingia nchini bila kibali.
“Wakiwa wamepakiwa kwenye gari lenye namba za usajili T. 824 DFG
aina ya Town hiace pickup lililokuwa likiendeshwa na Amiri Alalae
“alisema kamanda Lyanga.
Kamanda Lyanga alisema, wahamiaji waliingia nchini kwa njia ya majini wakitumia
majahazi na kushukia maeneo ya bandari bubu ya Jitu Kuu kutoka nchi jirani ya
Kenya.
Alisema watawakabidhi kwa idara ya uhamiaji ili waweze kuchukuliwa hatua
za kisheria.
Kamanda huyo alitoa rai kwa wananchi hasa madereva kuacha tabia ya
kusafirisha wahamiaji haramu kwa lengo la kujiongezea kipato.
Alisema kwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na kamwe hawatakuwa na
muhali na wale wote wanaofanya biashara hiyo ndani ya mkoa wa Pwani.
No comments:
Post a Comment