Timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri wa
chini ya miaka 17 maarufu kama Serengeti Boys, inatarajiwa kusafiri kesho saa
10.45 jioni kwa Ndege ya Shirika la Ndege la Emirates kwenda Morocco kupitia
Dubai, Falme za Kiarabu (UAE).
Timu hiyo yenye wachezaji 23 na viongozi wanane
watakuwa Uwanja Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu J.K. Nyerere kuanzia
saa 7.00 mchana kwani wanatakiwa kuanza kuingia uwanjani saa 7.45 kwani saa
tatu baadaye ndipo ndege itakapopaa.
Wanahabari wanaweza kupata mahojiano ya mwisho
kadhalika kupata picha za habari wakati huo wa mchana kabla hawajaingia ndani
kwenye ukaguzi wa taratibu za (check in logistics).
Kabla ya kusafiri, timu hiyo ilikuwa kambini hapa
nyumbani tangu Januari 29, mwaka huu na baada ya kambi ya mwezi mmoja na nusu,
ilicheza mechi tatu za kirafiki za kimataifa.
Machi 30, 2017 ilicheza Burundi ‘Intamba Murugamba’
na kushinda mabao 3-0 kabla ya kurudiana tena Aprili 1, mwaka huu na kushinda
mabao 2-0. Mechi zote mbili zilifanyika Uwanja wa Kaitaba, ulioko Bukoba mkoani
Kagera.
Mechi ya mwisho hapa nyumbani ilifanyika Aprili 3,
mwaka huu dhidi Ghana ‘Black Starlets’ na kutoka sare ya 2-2 katika mchezo
ulifanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Serengeti Boys ilitumia mchezo kama ishara ya
kuwaaga mamilioni ya Watanzania kabla ya kusafiri kwenda kwenye fainali za
Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana zitakazofanyika Gabon kuanzia Mei 14,
mwaka huu.
Serengeti Boys itakuwa Rabat, Morocco kufanya kambi
ya takribani mwezi mmoja kuanzia Aprili 5, mwaka huu. Ikiwa huko angalau itacheza
mechi za kirafiki zisizopungua mbili dhidi ya wenyeji morocco na timu nyingine
ya jirani ama Tunisia au Misri.
Kambi hiyo ya Morocco itamalizika Mei mosi, mwaka hu
ambako timu itasafiri hadi Cameroon. Ikiwa Cameroon, timu itacheza mechi mbili
za kirafiki za kimataifa dhidi ya wenyeji yaani Mei 3 na 6, mwaka huu kabla ya
kusafiri Mei 7, mwaka huu kwenda Gabon ambako Serengeti Boys imepangwa kundi B
pamoja na timu za Mali, Niger na Angola.
Vipimo vya mechi dhidi ya Ghana kadhalika hapo
baadaye Cameroon, vitakuwa mwafaka kwenye kufanya tathmini ya uwezo wa
Serengeti Boys kwani wapinzani hao wamekuwa na rekodi nzuri kwenye soka la
vijana na kwa kipindi hiki zimepangwa kundi A pamoja na wenyeweji Gabon na
Guinea.
No comments:
Post a Comment