Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa
Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72 imeipa Simba SC pointi tatu na
mabao matatu kutokana na rufaa waliyoikatia Kagera Sugar kwa kumtumia beki
Mohammed Fakhi akiwa ana kadi tatu za njano katika mechi baina ya timu hizo
Aprili 2, mwaka huu.
Katika mchezo huo ambao Kagera Sugar
walishinda mabao 2-1 Uwanja wa Kaitaba, wanadaiwa kukiuka kanuni kwa
kumchezesha Fakhi, beki wa zamani wa Simba badala ya mchezaji huyo kutumikia
adhabu ya kadi tatu za njano alizopata mfululizo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Ahmed
Yahya amewaambia Waandishi wa Habari usiku wa April 13, 2017 kwamba Kamati
ilibaini ni kweli Kagera Sugar walifanya kosa hilo la kikanuni na adhabu yake
ni kupokonywa ushindi.
Kwa ushindi huo, Simba sasa
inafikisha pointi 61 baada ya kucheza mechi 26, wakiendelea kuongoza Ligi Kuu
Tanzania bara mbele ya mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 56 wakiwa
wamecheza mechi 25.
Ikumbukwe Simba iliwasilisha
malalamiko ikitaka ipewe ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kutokana na
Kagera Sugar kumchezesha Fakhi akiwa na kadi tatu za njano katika mechi yao
namba 194 iliyofanyika Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Katika kikao chake awali Ijumaa
iliyopita, Kamati baada ya kupitia malalamiko hayo, iliahirisha shauri hilo
hadi leo (April 13, 2017) kujipa muda wa kufuatilia baadhi ya vielelezo kuhusu
malalamiko hayo.
“Malalamiko yaliletwa kwetu na timu
ya Simba baada ya kufungwa na Kagera Sugar 2-1 kwenye uwanja wa Kaitaba, Simba
walileta malalamiko kwamba kuna mchezaji mmoja wa Kagera Sugar Mohamed Fakhi
alicheza mchezo huo wakati akiwa na kadi tatu za njano jambo ambalo ni kinyume
na taratibu zetu kwa mujibu wa kanuni zetu za ligi,” alisema mwenyekiti wa
kamati ya saa 72 wakati akitangaza uamuzi uliofikiwa na kamati yake.
“Tulikaa kikao cha kwanza siku ya
tarehe 7 April, 2017 tukajadili, bahati mbaya siku hiyo hatukufanikiwa kufikia
mwisho kwa sababu tulikuwa tunakosa baadhi ya taarifa ambazo zinaendana na
maamuzi ambayo tungeweza kuyafanya kwa hiyo tulijipa muda hadi leo na
tumefanikiwa kuzipata taarifa ambazo tulikuwa tunazitafuta na jioni hii
tumefikia maamuzi.”
“Kutokana na nyaraka tulizonazo
imethibitika kwamba, mchezaji huyu ambaye anaitwa Mohamed Fakhi alipata kadi ya
njano kwenye mchezo kati ya Kagera Sugar na Mbeya City, akapata kadi nyingine
ya njano kwenye mchezo kati ya Kagera Sugar na Majimaji na pia akapata kadi ya
njano kwenye mchezo kati Kagera Sugar na African Lyon.”
“Baada ya kupata malalamiko haya, watu
wa Kagera Sugar walikuja juu na kusema kwamba, mchezaji wao alipewa kadi kwenye
mchezo kati ya Kagera Sugar na African Lyon na huo ndio utata uliotufanya
tutafute ushahidi kuona kwamba hicho kitu kilitokea. Tumepata taarifa na kamati
imeridhia kwamba hiki kitu kilitokea na kutokana na hilo, mchezaji huyo alikuwa
nje ya sheria 37 (14) na adhabu yake ipo kwenye sheria yetu ambayo inasema
kwamba (timu itakayotumia mchezaji ambaye ana kadi tatu za njano, basi
itabatilishiwa matokeo na kunyang’anywa ushindi. Timu pinzani itapewa ushindi
wa pointi na magoli matatu).”
Kwa hali hiyo, naomba nitangaze rasmi
kwamba, kamati imefikia maamuzi hayo na taratibu zingine zitafuata kuhusiana na
hilo.
Tumechukua muda mrefu kutoa maamuzi
kwa sababu ya hali ilivyokuwa, kwamba upande wa pili walikuwa wanasema rekodi
zao hazioneshi hivyo kwa hiyo ilibidi tutafute rekodi za ziada ndiyo maana
tumechukua muda mrefu kutoa maamuzi ya suala hili. Vinginevyo tungetoa maamuzi
siku
ya tarehe 7
tulipopata malalamiko haya.
No comments:
Post a Comment