Tanzania inatarajiwa kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuwa na reli ya
kisasa inayotumia umeme na mafuta itakayokuwa na uwezo wa kusafiri masafa
marefu kwa mwendokasi wa kilometa 160 kwa saa.
Akizungumza katika uwekaji wa jiwe la msingi wa awamu ya kwanza ya ujenzi
wa reli hiyo ya leo huko Pugu nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alisema kuwa reli hiyo
itakuwa ya kisasa zaidi barani Afrika na itasaidia kukuza uchumi wa nchi kwa
kuchochea fursa za biashara ndani na nje ya nchi.
Awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo ambayo itahusisha kipande cha
kilomita 300 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro utagharimu jumla ya shilingi
trilioni 2.8 na utatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 30.
Dkt Magufuli alitoa mfano wa nchi zenye reli za mwendokasi lakini masafa
mafupi barani Afrika kuwa ni Morocco ambayo inasafiri kwa mwendokasi wa
kilomita 220 kwa saa na Afrika Kusini inayosafiri mwendokasi 150 kwa saa.
Dkt Magufuli alieleza kuwa baada ya kukamilika kwa mradi huo Tanzania
itakuwa nchi ya kwanza kuwa na treni itakayosafiri masafa marefu kwa mwendokasi
wa km 160 kwa saa.
Alifananua kuwa mradi huo wa ujenzi wa reli unatekelezwa kwa fedha za
Tanzania ambapo tayari serikali imeshawalipa wakandarasi malipo ya awamu ya
jumla ya shilingi bilioni 300.
Akizungumzia umuhimu wa ujenzi wa reli hiyo, Rais Magufuli alisema kuwa
reli hiyo itasaidia kuongeza kasi ya usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya
Dar es Salaam kwa haraka na kuwafikia wateja ndani ya muda mfupi.
Vilevile, reli hiyo itarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo pamoja
na kukuza biashara kati ya Tanzania na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo DRC, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudani ya Kusini.
Sambamba na hayo, Rais Magufuli alisema kuwa ujenzi wa reli hiyo
utasaidia kuimarisha sekta nyingine za uchumi ikiwemo utalii, viwanda, kilimo,
pamoja na kutoa ajira kwa watanzania ambapo kutakuwa na ajira muda zipatazo
600,000, na ajira za kudumu 30,000.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa
Makame Mbarawa alisema kuwa reli hiyo ya kisasa inayojengwa na wakandarasi
kutoka muungano wa kampuni mbili za nchi ya Uturuki na Ureno
itakuwa na uwezo wa kusafirisha mizigo tani 10,000 kwa mara moja na
kutumia saa 2 kutoka Dar es salaam hadi Dodoma na saa 7 na dakika 40 kutoka Dar
es Salaam hadi Mwanza.
Naye, Mjumbe wa Bodi ya Kampuni ya ujenzi kutoka Uturuki ya Yapi Merkezi
Bw. Emre Aykar alisema kuwa reli hiyo itaimarisha zaidi uhusiano wa Uturuki
na Tanzania na kuongeza kiwango cha shughuli za biashara nchini.
“Tunaahidi kujitahidi kumaliza mradi kwa wakati na katika kiwango
kinachotakiwa” alisema Bwana Aykar.
Reli hiyo ya kisasa inatarajiwa kujengwa pembeni ya reli ya kati ambayo
ilijengwa wakati wa utawala wa kikoloni wa Wajerumani na Waingereza miaka 112
iliyopita.
No comments:
Post a Comment