Tanzania inategemea kupata Megawati 400 za umeme kutoka Ethiopia ikiwa ni
moja ya makubaliano yaliyofikiwa baada ya ziara ya kikazi ya siku mbili ya
Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe.Haile Mariam Desalegn.
Hayo yamesemwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt John
Pombe Magufuli alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari juu ya makubaliano na
mikataba ambayo nchi za Tanzania na Ethiopia wametiliana saini leo Ikulu Jijini
Dar es Salaam.
“Tukitaka kujenga uchumi wa viwanda ni lazima tuwe na umeme wa
kutosha,wenzetu Ethiopia wametuonyesha njia na mimi nimemuomba Mhe.Waziri
atusaidie wataalamu kutoka nchini kwake ili waje tuwaonyeshe maeneo
mbalimbali watusaidie katika kupata umeme wa uhakika kwa kujenga mabwawa ya umeme
ambayo yamesaidia sana katika kupatikana kwa umeme wa kutosha nchini
kwao.”Aliongeza Rais Magufuli.
Aidha amesema kuwa kupatikana kwa umeme huo kutasaidia kuleta changamoto
kwa shirika la umeme nchini katika kuwapatia wananchi bei ya chini na hivyo kuleta
ushindani katika upatikanaji wa umeme nchini.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe.Haile Mariam Desalegn amesema
kuwa wana mengi ya kujifunza kutoka Tanzania kwani nchi hizi mbili zina
historia inayofanana na kuongeza kuwa hakuna haja ya wao kwenda nje ya Afrika
kupata uzoefu katika masuala mbalimbali.
Ameongeza kuwa lengo kuu la kuja nchini ni kwa sababu anahamini nchi hizi
mbili zinaweza kuunganisha nguvu zake na kuwa nguzo kuu katika maendeleo katika
eneo la ukanda wa Afrika Mashariki na kati.
“Tanzania na Ethiopia ni nchi ambazo zina ushirikiano mzuri sana,sisi sio
washindani bali tunasaidiana katika masuala mbalimbali kwani tumekuwa katika
hatua mbalimbali za kuwaondoa wananchi wetu katika umaskini katika hatua
zinazofanana,na huu ni wakati muafaka katika kuimarisha ushirikiano wetu kwa
faida ya watu wetu kwa ujumla”Alisisitiza Mhe.Desalegn.
Aidha amesema kuwa mabadiliko ya kilimo
katika nchi zetu ndio msingi wa maendeleo
pamoja na utumiaji wa teknolojia bora
utasaidia katika maendeleo ya viwanda vidogo vidogo.
Viongozi hawa wamekubaliana kushirikiana kwa kubadilishana uzoefu juu ya
namna sekta mbalimbali zitakavyoleta manufaa ya kiuchumi zikiwemo huduma za
benki, madini na gesi, elimu na mawasiliano.
Ziara ya Waziri Mkuu Mhe. Haile Mariam Dessalegn imekuwa ya manufaa
makubwa kwa Tanzania na amesisitiza kuwa wakati umefika wa kukuza biashara kati
ya nchi hizi ambazo kwa sasa thamani ya biashara kati yake ni Dola za Marekani
milioni 2.24 tu.
No comments:
Post a Comment