Baadhi
ya wakazi wanaotumia barabara ya Vigwaza-Buyuni-Mwavi wakipita kwa shida kutoka
na barabara hiyo kuharibika vibaya kutokana na mvua.(picha na Mwamvua Mwinyi)
MBUNGE
wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete,akiangalia barabara kutoka Vigwaza-Mwavi
iliyoharibika vibaya eneo la Buyuni hali inayosababisha magari kushindwa
kupita.
Mkazi
wa Mwavi ,Zainab Zuberi akivushwa kwenye maji yaliyokata barabara eneo la
Buyuni,kwa kubembwa shingoni .
Mbunge
wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete,akizungumzia kero ya kuharibika kwa
baadhi ya miundombinu ya barabara kutokana na mvua zinazoendelea
kunyesha,ambapo mvua iliyonyesha april 7 na 8 imesababisha kuharibu barabara ya
Vigwaza-Buyuni-Mwavi na ya Milo-Kitonga-Ruvu.(Picha na Mwamvua Mwinyi)
..........................
Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
MVUA kubwa iliyoambata na upepo mkali,imekata
mawasiliano ya miundombinu ya barabara eneo la Buyuni, na kusababisha wakazi
kutoka kata ya Vigwaza na Mwavi jimbo la Chalinze,kupata shida.
Hali hiyo inasababisha wakazi
hao,kuvushwa kwa kupata msaada wa kubebwa mgongoni na shingoni kwa gharama ya
sh.3,000 na 2,000 na pikipiki kupitishwa kwa sh.5,000 huku magari yakishindwa
kupita kabisa.
Baadhi ya wakazi hao,akiwemo Zaina
Zuberi aliekuwa akienda Mwavi,alisema wapo katika hali ngumu .
“Mvua hapa bado haijanyesha,maji haya
yanatokea maeneo ya Msoga huko na kufika huku daraja la Mbiki,Buyuni na
kukatiza katika hii barabara,sipati picha mvua ikipiga hapa kwa mwezi huu”
“Barabara ni mbovu kama
mnavyojionea,haipitiki,watu tunapata shida kufuata mahitaji ya nyumbani ,tatizo
ni mkandarasi ,barabara imejengwa bila kuwekwa makaravati,kila akielekezwa
kujenga kutokana na hali halisi ya barabara haiwi hivyo,”
Nao baadhi ya vijana wanaosaidia
kuwavusha watu na pikipiki,akiwemo Rashid Juma,alisema tangu mvua ziharibu eneo
hilo april 7 wanavusha watu kwa maelewano kulingana na uwezo wa mtu.
“Tunapata fedha kulingana na kichwa cha
mtu au pikipiki,kila mtu mmoja 3,000 au 2,000 na pikipiki 5,000 “alieleza.
Aidha kutokana na mvua hizo,zimeathiri
pia barabara nyingine ya kutoka Milo-Kitonga hadi Vigwaza.
Mbunge wa jimbo la Chalinze ,Ridhiwani
Kikwete ,alitembelea barabara hizo na kujionea hali halisi.
Ridhiwani alisema ,hali iliyopo
hairidhishi na kuwapa wakati mgumu wakazi wa maeneo hayo,na ameahidi kuisimamia
kero hiyo kwa kuifikisha bungeni na halmashauri ya wilaya ya Chalinze ili
lifanyiwe kazi.
Alieleza kuna kila sababu ya mkandarasi
kufanya kazi kulingana na uhalisia wa eneo husika hali inayosababisha wananchi
kupata tabu na barabara kuharibika kila wakati.
Katika hatua nyingine Ridhiwani ,aliunga
mkono juhudi za ujenzi wa darasa lililobomoka kutokana na mvua iliyonyesha
april 7 ambapo amechangia kiasi cha sh.100,000,mabati 50,mifuko ya saruji 50 na
nondo 20.
Alibainisha kwamba shule hiyo imejengwa
miaka 40 iliyopita hivyo miundombinu yake pia imechakaa.
Ridhiwani alisema kuna kila sababu ya
kuangalia namna ya kukarabati shule hiyo kwani majengo yake yamejengwa miaka
mingi.
Afisa mtendaji wa Kidogozero,Lilian
Mbwa,alisema kila kaya itachangia matofali mawili na kila mjumbe wa serikali ya
kijiji ni tofali 10.
Hata hivyo alisema halmashauri ya kijiji
itachangia jumla matofali 200 na wadau wa maendeleo matofali 300.
Mwishoni mwa wiki iliyopita,kaya zaidi ya
20 zimekosa makazi ya kuishi na nyumba zaidi ya 90 ziliharibika ,kubomoka
na nyingine kuezuliwa mapaa huko jimbo la Chalinze,kutokana na mvua
iliyoambatana na upepo mkali.
Maeneo yaliyokumbwa na adha hiyo ni
Chalinze Mzee,Bwawa la umwangiliaji la Msoga ambalo limetoboka ,Msoga na shule
ya Sekondari ya Imperial.
No comments:
Post a Comment